
Dar es Salaam, Octoba 9, 2020: Msimu wa 11 wa mbio za Rock City Marathon zinazofanyika kila mwaka jijini Mwanza umezinduliwa rasmi hii leo jijini Dar es Salaam.
Waandaaji wa mbio hizo Kampuni ya Capital Plus International imesema kuwa mbio hizo zenye agenda ya kutangaza utalii wa ndani katika mikoa ya Kanda ya Ziwa zimepangwa kufanyika Novemba 29 mwaka huu eneo la Rock City Mall jijini Mwanza.
Akizungumza kwenye hafla fupi ya uzinduzi huo, Mratibu wa mbio hizo Bw Kasara Naftal alisema maandalizi muhimu yameshafanyika ikiwemo suala zima la fulana za washiriki pamoja na medali huku akitaja mbio zitakazohusishwa kuwa ni km 21, km 10 na Km 5.

“Kuhusu zawadi, pamoja na medali washindi wa kwanza wa mbio za kilomita 21 kwa wanaume na wanawake watajinyakulia sh. Mil 2 kila mmoja, sh.mil 1.3 /- kwa washindi wa pili na sh. 700,000 kwa washindi wa tatu, huku washindi wanne hadi kumi nao pia wakiibuka na zawadi za medali na pesa taslimu.’’
“Kwa upande wa mbio za Kilomita 10 hatutakuwa na zawadi za fedha taslimu isipokuwa washiriki watajipatia medali na tshirts . Kuhusu mbio za kilomita tano ambazo zitahusisha washiriki kutoka mashirika na taasisi mbalimbali (corporates) sambamba na washiriki wenye ualbino zawadi za fedha taslimu zitatolewa kwa washindi watatu wenye ualbino pekee,’’ alitaja.

Mbio za Rock City Marathon zilizoanzishwa miaka kumi na moja iliyopita zinazozidi kujiongezea umaarufu kila mwaka na tayari zimefanikiwa kuwavutia baadhi ya wadhamini ikiwa ni pamoja na kampuni za TIPER, Pepsi, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Kampuni ya Ujenzi ya CRJE, Pigeon Hotel, CF Hospital, Hospitali ya Bugando, Garda World, The Cask na Chuo cha SAUT Mwanza.
Kwa upande wake Msemaji wa mbio hizo Bw Samwel Gisayi alisema usajili wa mbio hizo tayari umekwisha anza kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya mbio hizo pamoja na usajili wa kawaida kupitia vituo mbalimbali vilivyopo mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Dodoma, Arusha huku mikoa zaidi ikiendelea kuongezwa.

“Usajili unaendelea vizuri na mwitikio wa washiriki ni mkubwa. Lengo ni kukimbiza washiriki wasiopungua 3000 yakiwemo makundi yote yaani wakimbiaji wa mbio za ushindani (Elite runners), washiriki wa mbio za kujifurahisha (Fun run) pamoja na wanafunzi,” alisema.