×

Guu la Mugalu Laekezwa Yanga SC

AKIPACHIKA mabao matatu mfululizo katika michezo ya Ligi Kuu Bara, mshambuliaji mpya wa Simba Mkongomani, Chris Mugalu amesema kuwa nguvu na akili zake ameziekeleza kwenye mchezo ujao dhidi ya Yanga.

 

Staa huyo mpya ndani ya Simba amefunga mabao akiwa amecheza michezo mitatu pekee kati ya mitano yote akitokea benchi wakati timu hiyo ilipocheza na Biashara United, Gwambina FC kabla ya kuvaana na JKT Tanzania.

 

Mkongomani huyo katika mabao yake hayo matatu, mawili alifunga kwa kuwachambua makipa kwa njia ya miguu walipocheza dhidi ya Biashara na Gwambina kabla ya kufunga kwa kichwa na JKT.

 

Kwa mujibu wa Mugalu malengo yake ni kuona akiendelea kufunga mabao katika kila mchezo wa ligi unaofuatia lengo kuipa timu yake matokeo mazuri ya ushindi pekee.

Mugalu alisema kuwa hicho ndicho kilichomleta Simba, hivyo ni lazima atimize majukumu yake ya ndani ya uwanja kwa kuhakikisha anatoa mchango katika timu ikiwemo kufunga na kutengeneza nafasi za kufunga mabao.

Aliongeza kuwa anafurahia muunganiko wa timu uliokuwepo kati ya viungo na washambuliaji katika kuipa ushindi timu yao huku akiahidi kuendelea kutumia vema kila nafasi anayoipata ya kufunga.

 

“Ninafahamu kilichonileta hapa Simba ambacho cha kwanza ni kufunga na kutengeneza nafasi za kufunga mabao pekee, hicho ndiyo ninachokiangalia kwa sasa katika timu yangu hii mpya.“Bila ya kuangalia ushindani wa namba uliokuwepo katika timu hivi sasa, mimi ninachoangalia ni kupambana kuhakikisha ninatumia kila nafasi ninayoipata katika kufunga mabao.

 

“Ninashukuru nimeanza vema kwa kufanikiwa kufunga mabao matatu katika michezo niliyocheza nikitokea benchi, hivyo ninajisikia furaha na malengo ni kuendelea na kasi hii ya kufunga mabao katika mchezo ujao dhidi ya Yanga, mimi siku zote nikimaliza mechi moja basi akili yangu inahamishia mchezo unaofuatia,” alisema Mugalu.

 

Aliongeza kuwa: “Ninapoingia kwenye mechi najiamini nitafunga na nisipofunga najisikia vibaya sana. Nikifunga najisikia vizuri sana, nitawafurahisha mashabiki zaidi kwa kufunga.”

Stori: Wilbert Molandi na Said Ally,Dar

Leave a Comment