×

B. Wine: Polisi Wameiba Nyaraka Uteuzi Wangu Urais

MWANASIASA na mwanamuziki wa Uganda, Robert Kyagulanyi, al maarufu Bobi Wine, ameliambia shirikala utangazajila  BBC kuwa nyaraka zinazohitajika kwa ajili ya uteuzi wake wa kugombea urais zimepotea katika ofisi yake baada ya uvamizi wa ofisi hiyo wa vikosi vya usalama siku ya Jumatano mchana.

 

Moja ya masharti ya wagombea ni kuwasilisha sahihi za wafuasi wao 100 waliojisajili kupiga kura kutoka katika walau theluthi mbili ya wilaya za Uganda.   Bobi Wine anasema timu yake ilikuwa tayari imekusanya sahihi milioni sita lakini hizi sasa zimepotea.

 

“Serikali ya Museveni inajaribu kunizuia kuteuliwa kama mgombea wa urais. Kuanzia kuhoji nyaraka zangu, kuhoji umri wangu- na sasa wanafanya kila juhudi kukwamisha uteuzi wangu na ninaamini kuwa ndiyo maana walichukua saini yangu.

 

“Hatutakata tamaa, tumekwisha ripoti mara moja kwa matawi yetu kuhakikisha wanaanza kukusanya saini mara moja na tunatumaini kufikia Ijumaa tutakuwa na saini zinazohitajika,” alisema.

 

Mbunge huyo alikuwa akizungumza na BBC baada ya kutoroka kutoka katika ofisi yake wakati makumi kadhaa ya askari na polisi walipowasili kufanya msako.

 

Pia alisema shilingi milioni 23 za Uganda ($6,200 ) zilichukuliwa. Anasema pesa hizi zilichangishwa kusaidia kulipia gharama za uchaguzi kwa ajili ya wanachama wanaotaka kugombea ubunge.

 

Polisi hawakujibu wito wa BBC wa kuzungumzia madai ya Bobi Wine. Awali walikana kuwa uvamizi wa ofisi yake ulichochewa kisiasa. Tume ya uchaguzi iliwapatia wagombea siku ya Ijumaa kuwa muda wa mwisho wa kuwasilisha fomu zao za uteuzi.

 

Msemaji wa tume anasema hawezi kuzungumzia juu ya madai ya Bobi Wine ya kutoweka kwa nyaraka lakini anasema muda wa mwisho unaweza kuongezwa kwa mgombea iwapo wataifahamisha tume rasmi.

 

Leave a Comment