×

Irene Uwoya: Ni Kweli Naogea Maziwa ya Ng’ombe!

IRENE Pancras Uwoya ni binti wa rubani mstaafu. Uwoya ni miongoni mwa mastaa wa Bongo Movies, wenye majina makubwa Bongo.

Kupitia sanaa ya uigizaji, jina lake limebaki kwenye chati kwa zaidi ya miaka kumi sasa.

 

Katika mahojiano maalum (exclusive interview) na gazeti bora la mastaa wa IJUMAA WIKIENDA, Uwoya anafunguka mengi, lakini kubwa zaidi ni juu ya kuishi maisha ya kifahari, kufuru za hapa na pale akidaiwa kuwa na pesa chafu, kumficha mwanaume wake na ishu ya kuogea maziwa.

 

Uwoya ambaye ni mama wa mtoto mmoja wa kiume aitwaye Krish, anasema kuwa, kikubwa anakichofanya sasa hivi ni kufanya mambo yanayoendana na umri wake kwani miaka hairudi nyuma;

IJUMAA WIKIENDA: Mambo vipi Uwoya? Mzima?

UWOYA: Salama kabisa, niambie mpya maana najua unazo za kutosha.

IJUMAA WIKIENDA: Umekuwa kimya sana siku hizi, shida ni nini?

UWOYA: Hapana, nipo tu, tunapambana na maisha kila kukicha.

 

IJUMAA WIKIENDA: Hata wewe unapambana na maisha? Mbona kuna watu wanasema sasa hivi wewe ni boss lady, hii imekaaje?

UWOYA: Watu tu wanajua kuangalia na kusema bila kujua ukweli wa mtu. Unajua umaridadi unaficha umaskini!

IJUMAA WIKIENDA: Kwa hiyo watu wanavyosema una pesa chafu ni kweli au siyo kweli?

UWOYA: Hapana, sina pesa kihivyo wanavyosema, bali Mungu hajaninyima vyote maishani, ameniachia akili ya kutafuta pesa siku zote.

IJUMAA WIKIENDA: Unavyosema huna pesa, mbona bado unaishi Masaki (Dar), sehemu ambayo watu wanaamini wanaoishi ni watu wanaojiweza na kodi unayolipa ni kubwa, inakuwaje?

 

UWOYA: Ni kweli kodi ya Masaki si mchezo, lakini ninaitafuta kwa udi na uvumba kwa kuchanganua akili yangu kila siku, siyo kwamba ninakaa tu, halafu hiyo kodi inakuja, hapana, ninajituma.

IJUMAA WIKIENDA: Nyumba unayoishi Masaki unalipa Dola za Kimarekani 2,000 (zaidi ya shilingi milioni 4 za Kitanzania) kwa mwezi na zaidi ya shilingi milioni 48 kwa mwaka, sasa si ni bora ungekusanya hizo pesa ujenge nyumba yako?

 

UWOYA: Huwezi kujua mipango ya mtu, lakini kingine kikubwa sana kwenye maisha yangu, sipendi kujinyima na kujitesa kwani maisha yenyewe ni mafupi sana.

IJUMAA WIKIENDA: Kuna madai kuwa hivi karibuni ulifanya upasuaji (plastic surgery) ya uso ili uonekane bado msichana mdogo, unazungumziaje hilo?

 

UWOYA: (kicheko) kwa kutafuta nini kama uzee na uje tu kwa sababu uzuri wangu upo tu na hata kama ningeshika mkongojo, huwezi kuacha kuonekana. Mfano mzuri mtazame tu mama yangu ndiyo utajua!

IJUMAA WIKIENDA: Kwa kipindi kirefu umemficha mpenzi wako na wala hujawahi kuonekana naye popote, je, unaogopa kuibiwa na nyakunyaku wa waume za watu au ni kwa sababu gani?

 

UWOYA: Wa kuniibia bwana hayupo na wala hajazaliwa, lakini siwezi kumuweka hadharani na sitamuweka kamwe kwenye mitandao, labda chumbani kwangu.

IJUMAA WIKIENDA: Miongoni mwa mastaa wanaotuhumiwa kuvaa vigodoro mara nyingi ili waonekane wana mzigo (kalio) mkubwa na wewe unatajwatajwa sana, je, ni kweli na wewe unavaa?

 

UWOYA: Mimi kuweka kigodoro ni kumkufuru Mungu kwa sababu sina tatizo lolote kwenye mwili wangu. Hao wanaosema wanaosema hivyo ninawapa pole sana. Unajua kuna wakati unajiuliza kwa nini watu wana wivu wa kupitiliza?

IJUMAA WIKIENDA: Kumekuwa na gumzo kubwa juu ya kauli yako kuwa, huwa unatumia maziwa ya ng’ombe kuogea, je, ni kweli na bado unafanya hivyo?

 

Uwoya: Ni kweli nafanya hivyo, naogea maziwa na ndiyo maana sura yangu kila ninayeonana naye ananisifia. Mimi sipaki chochote, kikubwa zaidi ni hayo maziwa.

IJUMAA WIKIENDA: Krish amekua mkubwa sasa, je, una mpango wa kuongeza mwingine?

UWOYA: Nina hamu sana, tena sana. Natamani kupata mtoto wa kike, inabidi niongee na baby wangu, tufanye mambo kwa kweli.

 

IJUMAA WIKIENDA: Marafiki zako miaka yote ni walewale, sijaona ukibadilisha, nini siri yako?

UWOYA: Mimi ndivyo nilivyo, siwezi kubadilisha marafiki kwa sababu nilionao wananifaa kwa kila kitu.

IJUMAA WIKIENDA: Ni kitu gani unakikumbuka kwa marehemu mumeo, Hamad Ndikumana?

UWOYA: Upendo wake kwangu na kwa mtoto wetu, namkumbuka sana kwa hilo.

 

IJUMAA WIKIENDA: Vipi kuhusu baa yako ya Last Menutes (ipo Sinza-Mori, Dar), ndiyo imekufa moja kwa moja?

UWOYA: Hapana, hivi karibuni tunaifungua tena, itakuwa nzuri sana.

IJUMAA WIKIENDA: Uwoya nashukuru kwa ushirikiano wako…

Uwoya: Asante, karibu tena na tena.

MAKALA | IMELDA MTEMA, BONGO

Leave a Comment