×

Vikwazo Vya Silaha Iran Vyafikia Tamati

VIKWAZO  vya Umoja wa Mataifa (UN) vilivyopiga marufuku kuiuzia au kununua silaha kutoka Iran vimefikia tamati jana jumapili kama ilivyoafikiwa na mataifa za yenye nguvu kiuchumi na kivita licha ya Marekani kupinga mwisho wa marufuku hiyo.

 

Umoja wa Mataifa uliipiga marufuku Iran kununua silaha ikiwemo vifaru na ndege za kivita kutoka mataifa ya kigeni mwaka 2010 kufuatia msuguano uliozuka kuhusiana na mradi wake tata wa nyuklia, ambapo hapo kabla umoja huo uliweka vikwazo dhidi ya mauzo ya silaha kutoka Iran.

 

Taifa hilo la Kiislamu lenye misimamo mikali,  limeitaja hatua ya kufikia mwisho kwa vikwazo vya silaha kama “siku ya ushindi kwa jumuiya ya kimataifa, katika kupinga juhudi za utawala wa Marekani”.

 

“Hatua ya leo ya kurekebisha ushirikiano wa ulinzi kati ya Iran na ulimwengu ni ushindi katika mwelekeo wa mshikamano wa dunia, amani na usalama kwenye kanda yetu” ameandika Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Mohamed Javad Zarif, kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Ingawa Iran yenyewe inasisitiza kuwa haina mipango ya kununua silaha, kwa nadharia lakini Iran sasa inaweza kununua silaha inazotaka kuimarisha hazina yake ya  zana na mifumo ya ulinzi ambayo imekuwepo tangu Mapinduzi ya Kiislamu yalipofanyika mwaka 1979.   Pia nchi hiyo inaweza kuuza tena zana zote za kijeshi zinazotengenezwa na kampuni za ndani.

Aidha  serikali mjini Tehran inaweza kujaribu kununua mfumo wa ulinzi wa makombora wa S-400 kutoka Urusi pamoja na mifumo ya ulinzi mahsusi kwa ajili ya maeneo ya pwani.    China na Urusi ndiyo mataifa pekee ambayo yanaweza  pia  kuiuzia silaha Iran.

Leave a Comment