×

Adam Adam Tishio Jipya Ligi Kuu

MSHAMBULIAJI wa timu ya JKT Tanzania, Adam Adam, amewafunika mastraika wazawa na wageni baada ya kufunga mabao sita kwenye Ligi Kuu Bara akiwa mzawa wa kwanza kufikisha idadi hiyo msimu huu.

 

Adam pia ameweka rekodi ya kuwa straika pekee aliyefunga hat trick msimu huu ambapo alifanya hivyo dhidi ya Mwadui FC kwenye ushindi wa mabao 6-1 ukiwa ni ushindi mkubwa kwa timu hiyo msimu huu.

 

Sasa nyota huyu yupo kileleni kwenye chati ya ufungaji, akiwa na mabao sita sawa na Mzimbabwe, Prince Dube wa Azam FC.

 

Akizungumza baada ya mchezo dhidi ya Namungo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 huku yeye akifunga mabao yote mawili ya timu yake, Adam amesema: “Najisikia furaha kuendelea kufunga mabao mengi kwa ajili ya timu yangu, nafasi tuliyopo kwenye ligi si nzuri sana, hivyo inatubidi kupambana kwenye kila mchezo.

 

“Malengo yangu ni kuwa mfungaji bora msimu huu, hivyo inanibidi kupambana kwenye kila mechi nihakikishe nafunga mabao mengi zaidi.”

Adam amewapiku John Bocco, Yusuph Mhilu na Meshack Abraham wenye mabao manne kila mmoja.

 HUSSEIN MSOLEKA, Dar es Salaam

 

Leave a Comment