Marco Mzumbe, Dar es Salaam MAKOCHA wa Yanga na Simba wanaamini vikosi vyao kwa asilimia zote vimekamilika na viko fiti kisaikolojia kwa mchezo wa leo saa 11 jioni pale Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar.
Mrundi Cedric Kaze ambaye anaionoa Yanga na Mbelgiji Sven Vandenbroeck wa Simba, wamewataka mashabiki wao wawaombee dua njema kwani watapigana kufa na kupona kwenye mechi hiyo itakayorushwa live. Klabu hizo kongwe leo zitakuwa na kazi kubwa ya kuwadhihirishia mashabiki wao kuwa wako tayari kwa vita ya ubingwa na Simba ni mabingwa watetezi.
Makocha wote walipata fursa ya kupitia picha za video za wapinzani wao ambapo kila mmoja alifanikiwa kubaini mbinu mbalimbali wanazotumia wapinzani wao wanapokuwa ndani ya uwanja, lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha ushindi.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari jana, makocha hao kila mmoja alielezea namna alivyojipanga. Sven alisema: “Tunaenda kucheza na Yanga ya tofauti na msimu uliopita. Sasa wana kocha mpya na wachezaji wengi wapya hivyo tumejiandaa kwa ajili ya kukabiliana nao kuhakikisha tunashinda.
“Katika mchezo wetu tunatarajia kuwakosa wachezaji kama Chama (Clatous), Meddie Kagere, Bernard Morrison na Gerson Fraga ambao ni majeruhi, (Championi linafahamu kuwa Morrison amefungiwa mechi tatu na TFF).
“Tunaenda kucheza na Yanga tukifahamu kuwa wametuzidi pointi nne hivyo tunahitaji ushindi ili tupunguze pointi,” alisema Sven. Naye nahodha wa Simba, John Bocco alisema wachezaji wamejiandaa vya kutosha kuhakikisha wanawafurahisha mashabiki wao kwa kupata ushindi dhidi ya Yanga leo.
Kwa upande wake Kocha wa Yanga, Kaze alisema: “Tunafahamu ubora wa Simba ila kwa upande wetu tumejiandaa vyema na malengo yetu ni ushindi kwani kama tukishinda tutaongeza idadi ya pointi hivyo tunahitaji kufanya hivyo ili tuzidi kuwapita pointi nyingi na kifupi tupo tayari kwa mapambano.
“Katika mchezo wetu huu tunatarajia kuwakosa Haruna Niyonzima, Carlos Carinhos, Balama Mapinduzi na Adam Kiondo kwa kuwa ni majeruhi. Kuwakosa wachezaji hawa kutatupunguzia kitu lakini naamini waliopo watapambana kuhakikisha tunashinda.”
Naye nahodha wa Yanga, Lamine Moro alisema: “Naomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuiunga mkono timu kwani sapoti yao ndiyo itasaidia kutupa ushindi kesho (leo).”
