MBUNGE wa Kawe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Askofu Josephat Gwajima, amesema wabunge wengi wa chama hicho wameshinda kutokana na utendaji wa Rais John Magufuli katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kuongeza kuwa ushindi wa Magufuli wa kimbunga umeonyesha wazi kesho inang’aa kuliko jana.
Amesema hayo leo Ijumaa, Novemba 13, 2020 wakati akizungumza kwa niaba ya wabunge mara baada ya Rais Magufuli kufungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusema kuwa kuna maeneo wagombea walikuwa hawahitaji kupiga kampeni, bali walitaja tu jina la Magufuli na kura wakapata.
“Hotuba ya Mheshimiwa Rais ni hotuba ambayo akili ya kawaida ya binadamu haiwezi kuibeba, unless umepata ufunuo kutoka kwa Mungu, kwa sababu hiyo inanipelekea kusema shukrani kwako wewe Mheshimiwa Spika ulivyochaguliwa kwa kura nyingi na akaidhihirishia dunia kuwa muelekeo wake ni salama.
“Mheshimiwa Rais kazi yako nzuri imesaidia Wabunge wengi kuingia Bungeni, na hakika Bungeni wote walioingia ni watu bora hupati shida sana kufanya vetting wakati wa uteuzi chukua mtu yeyote piga naye kazi, umewapa likizo watu wa vetting hawana kazi kubwa. Sisi wabunge tulioingia Bungeni kwa mara ya kwanza performance yako ya miaka mitano, imetubeba, bila shaka tumepata kura kupitia wewe, ulikuwa tofali la ushindi wetu, kuna sehemu hatukuhitaji kupiga kura, tulitaja jina lako tu.
“Wabunge wote ni majabali hakuna mbunge mnyonge hata mmoja, umewapeleka likizo isiyo na malipo watu wa vetting kwa sababu kutoka Kaskazini mpaka Mashariki wabunge wote wanafaa kwa ajili ya kuitumikia serikali yako. Nikiri wazi hakuna beberu atakayekupenda kwa projection hii uliyoipanga, kwa mara ya kwanza kwenye historia ya nchi yetu kuweza kujitegemea ku-finance uchaguzi wake na kuizuia fedha inayotoka nje inayotupa masharti.
“Mhheshimiwa Rais uliposema utaruhusu maduka ya dawa za kienyeji, Mheshimiwa Nape hapa akawa ananikonyeza kwamba inawezekana na ungo za kupaa za wachawi zitaruhusiwa, nikamwambia hapana, Mheshimiwa Rais kwa kazi yako nzuri tumepata kura kupitia wewe, ulikuwa tofali la ushindi wetu.
“Jana Spika wakati anakaribisha wageni alisema Wasukuma washamba, nikakumbuka Mwl. Nyerere alipokuja Dodoma aliwaambia Wagogo panueni mashamba, wao hawakuelewa badala ya kupanua mashamba wao wakapanua masikio. Jamani Spika ni mtani wangu, msiwe na wasiwasi.
“Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Winston Churchill, aliwahi kusema ukiwa unasafiri ukawa unamtupia jiwe kila mbwa anayebweka hutofika safari yako, Mheshimiwa Rais waache mbwa wabweke sisi tuendelee na safari yetu ya kutimiza ilani, waache wabweke kwa raha zao wewe kaza mwendo,” amesema Gwajima.
Kwa upande wake, Spika Ndugai amesema; “Mheshimiwa Rais kwa kweli hili Bunge la 12 limesheheni watu wa kila aina, ungekuwa na muda nikupe demo ya wabunge kama 20 hapa nipigepige waongee hapa. Mheshimiwa Rais wengi tuna deni kwako na wengi ulipita ukasema nileteeni huyu.”
Spika Ndugai ameahirisha shughuli za Bunge hilo hadi Februari 2, 2021.

