×

JPM: Hakuna Uhuru, Haki Usio na Wajibu, Kosoeni kwa Hoja – Video

RAIS  John  Magufuli amesema kuwa siku zote uhuru unakwenda na haki pamoja na uwajibikaji hivyo serikali yake itahakikisha mambo hayo yanazingatiwa wakati wa kutekeleza na kukuza demokrasia nchini katika kipindi chake cha miaka mitano ijayo ya uongozi.

 

Amesema hayo leo Novemba 13, wakati akifungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jijini Dodoma na kuonyesha dira ya miaka mitano ya serikali yake ambapo imejikita katika kuboresha uchumi na maisha ya wananchi wake ikiwemo kurahisisha mambo mbalimbali katika sekta ya uwekezaji na biashara sambamba na kuweka miundombinu madhubuti ya anga, majini na barabara ili kuvutia uwekezaji na kurahisisha biashara pamoja na huduma za kijamii.

Badhi ya dondoo muhimu katika hotuba yake hizi hapa:

“Miaka mitano ijayo tutaendeleza jitihada za kukuza na kuimarisha demokrasia, ningependa kukumbusha kuwa lengo la demokrasia ni kuleta maendeleo siyo fujo, hakuna uhuru au haki usio na wajibu,  vyote vinakwenda sambamba, najua nimeeleweka vizuri.

 

“Kutokuwa Wabunge wa Upinzani hatusemi muunge mkono kwenye kila kitu, la hasha. Penye kukosoa kosoeni ila mkosoe kwa tija, Spika niliona jana umewainua madereva wanawake Bungeni ningefurahi na wewe Spika uwe mfano uanze kuendeshwa na dereva mwanamke.

 

“Sina shaka kwamba Bunge hili litatoa ushirikiano wa kutosha kwa Serikali. Napenda niweke bayana, ninaposema tunaomba ushirikiano haimaanishi kwamba tunataka muunge mkono kila kitu, la hasha! Penye kukosoa kosoeni, lakini kwa hoja na kutoa mapendekezo.

 

“Tunakusudia kuviboresha vitambulisho vya wajasiriamali kwa kuviongezea picha ili wafanyabiashara wadogo watambulike na kuwawezesha kupata mikopo benki, lengo ni kufanya wakue kibiashara.

 

“Tutaendeleza sana, nafurahi kuona Wabunge wengine wasanii wapo Bungeni, na nawatakia kila la kheri Taifa Stars kwenye mechi yao na Tunisia leo, namtakia heri pia Hassani Mwakinyo ambaye anapambana leo, Watanzania tunataka ushindi tumechoka kushindwashindwa.

 

“Wakati wa ugonjwa wa Corona mbali na kumtanguliza Mungu tiba mbadala nazo zimesaidia sana, miaka mitano ijayo tumekusudia kuimarisha kitengo cha utafiti wa tiba mbadala, hivyo sasa matibabu na maduka rasmi ya tiba za asili yataruhusiwa.

 

“Nilipokuwa kwenye kampeni, moja ya changamoto kubwa niliyoelezwa na wananchi ni shida ya maji, hususani maeneo ya vijijini, kwenye miaka mitano ijayo tutaelekeza nguvu zaidi katika kushughulikia suala la maji.”

 

Leave a Comment