×

Wasanii 6 wa Bongo Fleva Waliotikisa 2020

MUZIKI wa Bongo Fleva una wasanii wengi waimbaji; kazi yao ni moja tu, kutoa burudani kwa mashabiki wao ambao ndio wanunuzi wa bidhaa zao.

Kwa mwaka 2020 wasanii wengi wamefanya kazi nzuri kila mmoja kwa kiwango chake kutokana na malengo aliyojiwekea. Napenda kuangazia wasanii watano kutoka kwenye muziki huo ambao wametikisa mwaka 2020.

DIAMOND PLATNUMZ

Ni miaka mingi sasa amekuwa akifanya vizuri katika muziki huo, na amepachikwa jina la Chibu Dangote; kila mwaka amekuwa na ngoma ambazo zinafanya vizuri kwenye chati za muziki, mtaani na mtandaoni.

 

Mwaka huu 2020 alitumika na chama tawala – CCM katika kampeni zake. Ametoa ngoma nyingi zilizotikisa anga ya muziki kama vile Jeje, Gere aliomshirikisha Tanasha na kuwa na watazamaji (viewers) zaidi ya milioni 20 huko kwenye mtandao wa YouTube.

Huko nyuma amesumbua na albamu zake nyingi; kwa mfano albamu ya ‘A Boy From Tandale’ ikiwa ni albamu yake ya pili tangu alipotoka kimuziki mwaka 2009, ilitia fora.

 

Albamu ya A Boy From Tandale ilizinduliwa rasmi Machi 14, 2018 Nairobi nchini Kenya ambapo wasanii wote kutoka lebo yake ya WCB walishiriki pamoja na msanii kutokea Marekani, Omario ambaye pia ameshiriki kwenye wimbo wake unaokwenda kwa jina la African Beauty.

Diamond alifanya ziara (tour) kwa ajili ya kuitangaza albamu hiyo nchini Marekani kwa kipindi cha mwezi mmoja, wapenda muziki wa Afrika kutoka maeneo ya Texas, Los Angeles na Chicago walimpata mubashara kabisa Chibu Dangote.

 

NANDY

Licha ya nyimbo kama Subalkheri Mpenzi na Aibu alizotoa mwaka juzi, Nandy ameweza kutoa albamu yake ya kwanza tangu kuanza muziki, The African Princess ikiwa na nyimbo 13 ambayo alimshirikisha msanii mmoja pekee ambaye ni Aslay.

Albamu hii imeuzwa kwa mfumo wa nakala za kawaida (hard copy) pamoja na mtandaoni (streaming & downloads).

Mwaka huu ametoa ngoma kali kama vile Do Me, Dozi, Nanusu pia Acha Lizame na alishikiri kampeni kwa upande wa chama tawala.

 

Amefanya vizuri mwaka huu lakini huko nyuma aliwahi kushinda tuzo mbalimbali kama African Entertainment Awards (AEA) zilizofanyika Oktoba 20, 2018, New Jersey nchini Marekani.

Nandy alishinda kwenye kipengele cha Best Single Female kupitia wimbo wake uitwao Kivuruge ambao hadi sasa umepata viewers zaidi ya milioni 12 mjini YouTube.

Huyu ndiye msanii pekee wa kike kutoka Tanzania kushinda tuzo hiyo mwaka 2018. Nandy pia amewahi kushiriki tamasha la One African Music, Dubai. Amefanya show kadhaa za mafanikio nchini Marekani.

HARMONIZE

Mwaka huu umekuwa wa mafanikio makubwa sana kwa Harmonize kimuziki ukilinganisha na miaka mingine, ametoa nyimbo ambazo zimefanya vizuri zaidi kama vile Matatizo, Nimeshachoka, Happy Birthday na pia huko nyuma ameweza kushirikiana na wasanii wakubwa kutoka Tanzania na mataifa mengine ya Afrika.

 

Muimbaji huyo ambaye ndiye msanii wa kwanza kusaini kwenye lebo ya Diamond Platnumz ‘WCB’ mwaka 2018 ameweza kufanya kolabo na wakongwe wa Bongo Fleva kama Dully Skyes na Professor Jay ambao wote wawili walishawahi kufanya kazi na Diamond na kufanya vizuri.

 

Ana lebo yake iitwayo Kondegang ambayo tayari imesaini wasanii wake akiwemo Country Wizzy.

Pia amefanya kazi na wasanii wakali kutoka Afrika kama Eddy Kenzo (Uganda), Marina (Rwanda), Willy Paul (Kenya), Sarkodie (Ghana). Wengine ni Emma Nyra, Skales, IYO na OmoAkin, wote kutokea Nigeria.

 

Ngoma yake inayokwenda kwa jina la Kwangwaru aliyomshirikisha Diamond unatajwa kama wimbo wenye mafanikio makubwa zaidi kwenye Bongo Fleva. Ulitazamwa zaidi kwenye mtandao wa YouTube kati ya nyimbo zake, hadi sasa una viewers zaidi ya milioni 72.

Ngoma ya Harmonize iliyokuwa ikiongoza kutazamwa zaidi YouTube ni ‘Bado’ ambayo pia alimshirikisha Diamond na umefikisha viewers zaidi ya milioni 20.

Harmonize amewahi kufanya ziara ya kimuziki nchini Marekani kwa kipindi cha takriban mwezi mmoja ambapo alifanya show zake Houston TX, Dallas TX, Oakland CA, Seattle WA, Atlanta GA, Los Angeles CA, Private Event na Washington DC.

MBOSSO

Huyo ni msanii wa lebo ya WCB, alisaini Januari 27, 2018 kuitumikia. Alitoa ngoma yake ya kwanza inayokwenda kwa jina la Watakubali.

Ni baada ya kuvunjika kwa kundi la Yamoto Band ambapo kila msanii wa kundi hilo alianza kutoa kazi zake binafsi (solo project). Mbosso ndiye alikuwa msanii wa mwisho kutoa wimbo baada ya wenzake kumtangulia, hata hivyo amekuwa mwenye mafanikio makubwa zaidi.

Amefanya ngoma kali mwaka huu 2020 kama vile Nadata, Haijakaa Sawa, Sina Nyota na Shilingi.

 

Lakini pia ameweza kufanya vizuri na ngoma zake kama Nadekezwa, Hodari, Nipepe na nyinginezo.

Ngoma hizo zote zina viewers zaidi ya milioni 5.5 kwenye mtandao wa YouTube.

Alifanya ngoma na Diamond iitwao Jibebe waliyofanya pamoja na Lava Lava, ni miongoni mwa nyimbo chache kali zilizosumbua kila kona baada ya kuuachia hewani.

ALIKIBA

Licha ya kutoa ngoma kadhaa na kufanya vizuri, ameweza kutambulisha wasanii kutoka kwenye rekodi lebo yake iitwayo ‘Kings Music’.

Kings Music ina wasanii kadhaa na Alikiba pia anafanya kazi na RockStar Africa. Julai, 2017 Alikiba alitangazwa kuwa miongoni mwa wamiliki wa kampuni ya Rockstar 4000 Music Entertainment Co & Rockstar Television ambayo kwa sasa inajulikana kama RockStar Africa akiwa kama Mkurugenzi wa Muziki na Vipaji.

 

Alikiba si msanii wa kutoa nyimbo kila mara, mwaka huu alitoa ngoma iitwayo Mshumaa na Mediocre zilizotikisa. Baadhi ya ngoma zake nyingine ni Seduce Me, Chekecha Chekecha, Aje, Kadogo, Mvumo wa Radi, Dodo wenye views zaidi ya milioni 4 na zote zimefanya vizuri.

Pia ameweza kufanya shoo kubwa ndani na nje ya Tanzania, moja wapo ni tamasha la Africa All Star Music Fest lilofanyika nchini Canada, mwaka 2018.

Alikiba alitumbuiza jukwaa moja na wasanii kama Yemi Alade, Falz The Bahd Guy, Sheebah, Dj Spinal, Zahara, Nonso Amadi na Nsoki.

ZUCHU

Zuchu, mtoto wa malkia wa taarab nchini Tanzania, Khadija Kopa ndio msanii ‘kinda’ katika lebo ya WCB inayoongozwa na Diamond Platnumz alitambulishwa Aprili 8, mwaka huu na Diamond ambaye ni mkurugenzi wa lebo hiyo.

Zuchu amewahi kushiriki shindano ya kusaka vipaji vya muziki barani Afrika mwaka 2016 liitwalo Tecno Own The Stage na kuzawadiwa Sh36 milioni baada ya kuwa mshindi wa pili.

Tayari Zuchu ameachia ngoma saba ikiwemo ‘Wana’ yenye views zaidi ya milioni 8.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka WCB, Zuchu amekaa zaidi ya miaka minne (4) akipikwa ndani ya kundi hilo kabla ya kutambulishwa rasmi katika soko la muziki la WCB. Kiukweli ana kipaji.

 

MAKALA: ELVAN STAMBULI

Leave a Comment