
MABONDIA Francis Miyeyusho na Deo Samweli leo Jumamosi wanatarajiwa kupanda ulingoni kumaliza ubishi katika pambano la Dar Boxing Derby.
Pambano hilo linalosubiliwa kwa hamu na wadau wa mchezo huo likiwa chini ya udhamini wa Gazeti la Championi, Global TV Online na kinywaji cha Smart Gin.

Mabondia hao jana Ijumaa walipima uzito katika Uwanja wa Las Vegas uliopo Mabibo Sokoni ambapo kila bondia alikuja na staili ya aina yake kwa lengo la kutambia mpinzani wake.

Championi ambalo lilikuwepo uwanjani hapo lilimshuhudia Miyeyusho alifika uwanjani hapo kibosi akiwa ndani ya prado wakati mpinzani wake Deo Samweli alitinga katika gari aina ya Noah.
Mabondia hao walitambiana kwa kila mmoja kudai kumkalisha mwenzake huku wakieana heshima ya kutoa upinzani wa kweli.
Utamu mwengine ulikuwa kwa Fadhali Majiha ‘Stoppa’ aliyetinga katika tukio hilo la kupima uzito akiwa ndani ya guta huku akisindikizwa na kundi la mashabiki wake wakati mpinzani wake Abdallah Zamba ambaye alikuja akiwa amebebwa juu ya mabega ya mashabiki wake.

Kwa upande wa Mukhusini Swalehe ‘Alkasusu’ yeye alikuja na bonge la shangwe kutoka katika kambi ya Nakoz iliyokuwa ikiongozwa na bondia mkali Mfaume Mfaume ikiwa na msafara wa magari saba yalikuwa na mashabiki wengi wakati mpinzani wake kutokea Mbezi, Gabriel Chola yeye alifika katika uwanja wa huo akiwa amevalia vazi la kimasai huku akiwa amebebwa juu ya mabega ya mashabiki wake.
Alkasusu alipata nafasi ya kutambia mpinzani wake kwa kumwambia anajua hapendi kula sana kwa kuwa ni mtoto wa mama hivyo amepenga kumpa adhabu ya kichapo kikali ili wakati mwengine awe anakula chakula bila ya kuambiwa na mama yake lakini kwa upande wa Chola alisema hana muda wa kupiga kelele kwa kwani atakuwa na kazi moja ya ya kumfundisha mpinzani wake ngumi.

Shomari yeye alisindikizwa na aliyekuwa mlinzi wa Diamond Platnumz, Mwarabu Fighter lakini ametamba kumaliza ubabe wa mpinza Hashimu Chisola ambaye hakutaka kuleta mbwembwe zote.
Mganga aloga hadharani

Katika hatua nyengine kundi la mashabiki wa Fadhali Majiha walikuja na shabiki mwengine aliyekuwa amevalia mavazi ya uganga huku akiwa na chungu kilichokuwa na moto ambacho alikitumia kuweka chumvi ya mawe iliokuwa ikiiungua kabla ya kuvunja nazi kwa madai ya kumtakia ushindi bondia wake.
Tiketi za pambano hilo zinaendelea kuuzwa kw bei ya Sh 3000 kawaida huku kwa upande wa VIP ikiwa Sh 5000.