
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Simon Sirro, leo Novemba 22, 2020 amesema jeshi hilo litavitokomeza vitendo vya kihalifu vinavyoendelea katika Mkoa wa Mtwara, kama ilivyofanya wakati wa mauaji ya raia katika Wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani.

Sirro ameyasema hayo akiwa eneo la Kitava mkoani humo, wakati akizungumza na wakazi na kueleza kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kutokomeza uhalifu huo na kusema waliohusika na matukio ya mauaji ya raia na uharibifu wa mali zao watachukuliwa hatua haraka iwezekanavyo.
IGP Sirro ameongeza kuwa, “Kimsingi ni kwamba, tumejipanga vizuri wananchi wetu waendelee kurudi kwenye yale maeneo waliyokimbia kule mpakani (mpakani mwa Tanzania na Msumbiji), tumeshajiimarisha, tutahakikisha hili tatizo litachukua muda mfupi kama ilivyokua kwenye tatizo la Kibiti na Ikwiriri ilivyochukua muda mfupi. Hawa wahalifu tutawashughulikia huko huko waliko”.