
DAR: Ama kweli ukijiona una shida wenzako wanashida kwelikweli ambazo wewe ndiye unayetakiwa kuwasaidia. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia mateso anayoyapata Mama mjane, Felister Gabriel Lisso (52) mkazi wa Mbagala Kizuiani Dar ambayo yanatoa machozi.
Akizungumza na mwandishi wetu Bi. Felister alisema awali alikuwa akiishi raha mustarehe na mumewe aliyekuwa mwanajeshi lakini kutokana na tatizo la kutozaa mume huyo alimuacha na kuoa mke mwingine.
Felister alisema mume huyo aliyeishi nae zaidi ya miaka kumi alimuacha bila kumpa chochote na kuoa mke mwingine ingawa kwasasa mume huyo ameshatangulia mbele za haki na kumfamnya awe mjane ingawa alishaachwa.
Tangu alipoachika Bi Felister alikuwa akiishi kwa kutembeza mboga mitaani lakini hivi karibuni alianza kuugua na kila alipotumia dawa za kutuliza maumivu hayakuweza kutulia.
Kufuatia maumivu hayo makali alikwenda Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dar ambapo alipimwa na kubainika kuwa figo yake ya kushoto imevimba na ana uvimbe mwingine kwenye kizazi.

Kuanzia hapo alikuwa tayari ameshaelemewa na maumivi na kushindwa kufanya biashara yake ya kutembeza mboga mitaani.
Mjane huyu alisema katika familia yao walizaliwa saba lakini wenzake wote wamefariki na kumuacha peke yake na wazazi wake walishafariki siku nyingi hivyo anapata shida ya chakula na mahitaji mengine. Mjane huyo anaeleza;
“Hospitalini baada ya kulibaini tatizo langu walianza kuniandikia vipimo vingine vya kwenda kupima lakini kila kipimo nlichoandikiwa niliishia kuzihifadhi ndani hizo karatasi kwa kukosa pesa ya vipimo na sina hata bima.
“Kitakachoniua haraka ni njaa maana hapa unaponiona jioni hii tangu asubuhi nilipewa shilingi 200 na mtoto aliyepita hapo mlangoni kwangu hiyohiyo nikamtuma akaniletee mihogo miwili ya kukaanga na ndiyo niliyotia tumboni na nnayotegemea kulalia.
“Nawaomba Wasamaria wema wanisaidie matibabu kama kuna daktari mwenye hospitali yake, muuguzi au msamaria mwema yeyote aliyeguswa na tatizo langu naomba anisaidie msanii wa chakula au matibabu namba namba yangu ya simu ni 0711673618 jina Jane Funga”. “Naomba mnisaidie ndugu zangu Mungu ndiye atakayewalipa. Alimaliza kusema mjane huyo.
HABARI; Richard bukos, Uwazi