
BARAZA la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA) wameandamana katika ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizopo Kinondoni jijini Dar es Salaam kushinikiza kufukuzwa kwa wabunge wa viti maalum walioapishwa hivi karibuni wakiongozwa na Halima Mdee.

Juzi Jumatano, Chadema kupitia kwa Katibu Mkuu wake, John Mnyinka, kilisema hakiwatambui wabunge hao wanawake 19 wa viti maalumu wa chama hicho wakiwemo Halima Mdee, Esther Matiko, Esther Bulaya na wengine walioapishwa Novemba 24, 2020 na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, jijini Dodoma kwa madai kuwa wameapishwa bila ridhaa ya chama hicho.

Chadema ilitoa wito wa kuwataka wabunge hao kufika katika ofisi hizo leo Ijumaa, Novemba 27, asubuhi ili kuhojiwa na Kamati Kuu ya chama kutokana na kitendo walichokifanya.