
WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Afrika, Namungo, inatarajiwa kushuka dimbani saa moja usiku leo Novemba 28 kwenye dimba la Chamazi, Mbagala, Dar es Salaam kuvaana na klabu ya Al Rabita kutoka Sudan Kusini kwenye kombe la Shirikisho Afrika.
Kuelekea kwenye mchezo huo ambao ni wa hatua ya awali ya mtoano kuwania kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya kombe la shirikisho Afrika, Afisa Habari wa Namungo, Chindamba Namlia, amesema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na dhamira yao ni kupata ushindi nyumbani.
“Maandalizi ya mchezo wetu dhidi ya Al Rabita yamekamilika, wachezaji wako kwenye hali nzuri, morali ipo juu, tunawaheshimu wapinzani wetu lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda nyumbani ili iwe rahisi kwenye mechi ya marudiano ugenini,” amesema Namlia.
Naye kocha wa Namungo, Hemed Suleiman ‘Morocco’, amesema licha ya kukosa CD za kumsaidia kumuonyeshea video za marudio ni namna gani wapinzani wake wanacheza ili iwe rahisi kuwakabili, amesema bado anaamini maandalizi yao yatawasaidia kufanya vizuri kwenye mchezo huo.