![]()
KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhandisi Joseph Nyamhanga; Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimeti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurean Ndumbaro; na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo, jana Novemba 30, 2020, wametoa ufafanuzi juu ya hoja mbalimbali zilizojitokeza kwenye ajira mpya za waalimu.
Ufafanuzi huo umetolewa leo katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI – jijini Dodoma baada kutokea hoja mbalimbali katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuhusu ajira mpya za walimu zilizotangazwa hivi karibuni.
Nyamhanga amesema hoja kubwa ilyojitokeza ni kwa jina la mwalimu mmoja kujitokeza katika kila ukurasa na kuonekana mara 196, badala ya mstari wa maelezo ya Jedwali (sub- titles) lakini shule aliyopangiwa ni moja, pamoja na jina hilo kujirudia halikuchukua nafasi ya mwombaji yoyote ya walimu waliotakiwa kuajiriwa au kuathiri idadi ya waalimu waliotakiwa kuajiriwa na tayari marekebisho yamefanyika.
Amefafanua pia kuwa shule binafsi kupangiwa mwalimu, serikali imekuwa ikiingia ubia na baadhi ya shule binafsi ambazo hupokea wanafunzi wenye uhitaji maalum, shule hizo hupangiwa walimu na kupewa ruzuku ya uendeshaji, hivyo Shule ya Mwalimu Tutuba ilikuwa katika mchakato wa kuingia ubia na serikali lakini haukukamilika, hivyo serikali baada ya kujiridhisha mwalimu aliyepangiwa katika shule hiyo amepangiwa katika shule ya sekondari Malagarasi.
Kwa upande wa wahitimu waliomaliza kidato cha nne mwaka 2017, 2018 na 2019 kupangiwa vituo vya kazi, ameeleza waombaji wa ajira walitumia mwaka wa kuhitimu chuo badala ya mwaka wa kuhitimu kidato cha nne ambapo waombaji 27 waliandika mwaka 2019, waombaji 27 waliandika mwaka 2019 na waombaji 13 waliandika mwaka 2017, hivyo serikali ilihakiki vyeti vyao na kubaini kuwa waombaji hao walihitimu kidato cha nne kati ya mwaka 2010 hadi 2014.
Aidha amewalekeza wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa kuhakiki vyeti halisi vya waliopata ajira na kujiridhisha kabla ya kutoa barua za ajira, na kusisitiza kuwa endapo itabainika kuwepo udanganyifu au kasoro za vyeti vya kitaaluma wahusika watachukuliwa hatua za kisheria.