×

Ujio wa Pili wa Mzee Yusuf Umebuma?

MAPEMA mwaka huu, Mfalme wa muziki wa Taarab Bongo, Mzee Yusuf alirejea mjini kwenye muziki huo wa kidunia baada kuachana nao kumrejea Muumba kwa miaka kadhaa.

 

Baada ya muziki wa Taarab kuanza kupoteza mwelekeo, baadhi ya mashabiki walisema kuondoka kwa Mzee Yusuf ndiyo sababu ya kupotea muziki huo. Mashabiki wengine walikwenda mbali zaidi na kusema jinsi muziki wa Dansi ulivyopotea baada ya kifo cha Ramadhani MasanjaBanzastone’ ndivyo Taarab ilivyopotea baada ya kuondoka Mzee Yusuf.

 

Wengi wakiwa na fikra hizo vichwani mwao mapema mwaka huu Mzee alirudi mjini tena kwa mbwembwe zote na kufanikiwa kuujaza Uwanja wa Taifa wa Burudani wa Dar Live uliopo Mbagala Zakhem jijini Dar. Kujaa kwa umati ule kwa mashabiki wengi walijua sasa Mzee amesharudi na Taarab yake sasa tuanze kupata vitu vipya kama ilivyokuwa hapo awali.

 

Jamaa kukicha alikuwa haishiwi vionjo vya kunogesha mashabiki wake ukiusikilizia wimbo wa Mapenzi Chocolate kabla hujakaa sawa katoa, Anajua Kupenda, ukisema huo ndiyo bora mara katoa My Valentine ukisema huu hauna mpinzani, mara kakupa Daktari wa Mapenzi, hujakaa sawa mara V.I.P ukisema na huu mkali kuliko zote, mara unakuta kaachia Zibeni Njia Sio Ridhiki.

 

Nyimbo hizo zote zilikuwa hazipishani kufi kia mwaka ilikuwa ni ndani ya miezi kadhaa kaachia kitu utamu kama fundo za muwa, ukianzia juu kuja shinani.

 

Kwa hiyo baada ya Mzee Yusuf kurudi mashabiki walitegemea uhondo kurudi lakini matokeo yake imekuwa kimya sana zaidi ya wa kuwasikia vijana wa lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) chini ya Diamond Platniumz wakiachia vitu vikali kila kukicha.

 

Kufuatia hali hiyo wengi wamekuwa wakijiuliza sababu ya Mfalme huyo kurudi mjini kwa mbwembwe tena siku hiyo alipanda jukwaani akiwa na matikiti maji, mihogo, viazi, ndizi, zambarau na mazagazaga mengine akiwaaminisha mashabiki wake kuwa kweli amerudi mjini lakini tangu arejee amekuwa akiishi kimyakimya.

 

Mimi mwandishi wa burudani shoo nilizozishuhudia za Jahazi ni katika kumbi za pembezoni mwa Jiji la Dar kama zile za Monie Pub Kiwalani na nyinginezo.

 

Katika kumbi za katikati ya jiji alizokuwa akitumbuizakama vile ukumbi wa Travertine Magomeni, Kinondoni na kumbi nyingine kama hizo huenda bado anatafakuri maana mjini hawaingii kichwakichwa lazima uwe na taimingi kama Mzee Kombe.

 

Pamoja na kimya hicho lakini jamaa sio kwamba yupo kimya kabisa ameshatoa nyimbo mbili mpya; Narudi Mjini na Msinifokee lakini ujio wake sio wa mbwembwe kama enzi anatoa Mapenzi Chocolate, V.I.P na nyinginezo za kipindi kile. Hata hivyo jamaa bado ni shujaa maana kuna makundi mengi ya Taarab sasa hivi yanapumulia mashine angalau yeye anajaza mashabiki kimtindo huko pembezoni anakopiga.

 

Hivi karibuni niliongea na Mzee Yusuf kwenye onesho la pili alilofanya ambalo alilitumia kulizindua upya kundi lake la Jahazi Modern Taarab ambapo wengine walisema huenda lingeitwa Safi na. Katika shoo hiyo muitikio wa mashabiki haukuwa mkubwa sana ambapo alichonijibu yeye kazi yake ni kupiga kazi tu kadiri ya uwezo wake haangalii wingi wa mashabiki.

 

“Mimi siogopi shoo hata kama mashabiki wako wawili mimi nakamua kwa uwezo wangu wote ilo la kutumbuiza mashabiki wachache mimi wala halinisumbui kichwa” alisema Mzee Yusuf. Makundi mengine ya Taarab yanayoonekana kuendelea kupambana ni pamoja na Vuvuzela Classic, East African Melody, Mashauzi Classic na Gusagusa Modern Taarab.

MAKALA: RICHARD BUKOS

Leave a Comment