×

Kaze Aweka Kikao cha Pointi Tisa Yanga SC

KOCHA Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze ametoa maagizo kwa nyota wa kikosi hicho kuhakikisha wanashinda michezo yote mitatu iliyosalia ya raundi ya kwanza na kuendelea kulinda rekodi yao ya kutopoteza mchezo wowote kati ya michezo 14 waliyocheza mpaka sasa.

 

Ushindi dhidi ya Ruvu Shooting umeifanya Yanga kufikisha pointi 34 zinazowafanya waendelee kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, huku wakisaliwa na michezo mitatu pekee dhidi ya Mwadui Desemba 12, Dodoma Jiji Desemba 16 na dhidi ya Ihefu Desemba 26, mwaka huu.

Akizun-gumza na Championi Jumatano,Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema: “Kwanza ni jambo la kujivu-nia kwetu baada ya kufanikiwa kucheza michezo yetu 14 ya kwanza bila kupoteza mchezo tukishinda michezo kumi na kutoa sare michezo minne.

 

“Tumebakiwa na michezo mitatu pekee ili kuweza kukamilisha michezo yetu 17 ya raundi ya kwanza na kuelekea michezo hiyo kocha, Cedric Kaze amekaa kikao na wachezaji wote na kuwaagiza kuhakikisha tunakusanya pointi zote tisa zilizosalia na kuendelea kulinda rekodi yetu ya kutopoteza mchezo.

“Tunajua haitakuwa kazi rahisi kwani kati ya michezo hiyo mitatu, michezo miwili dhidi ya Mwadui na Ihefu tutacheza ugenini na mchezo dhidi ya Dodoma Jiji pekee ndiyo tutacheza nyumbani.

 

“Hivyo tumejipanga kuhakikisha tunakusanya pointi hizo tisa na hatutaidharau timu yoyote kati ya hizo kwani tunajua nao wanajipanga kusaka ushindi,” alisema Saleh.Yanga kwa sasa wapo kileleni wakiwa na pointi 34 baada ya kucheza michezo 14, wameshinda michezo kumi, wametoka sare minne na hawajapoteza mchezo wowote.

Stori na Joel Thomas,Dar es Salaam

USIPIME! Huyo TADDEO LWANGA wa SIMBA ni HATARI, Cheki BALAA Lake MAZOEZINI…

Leave a Comment