
Dunia ikiwa siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia, Mkurugenzi wa Taasisi ya Agape, John Myola ambayo inayofanya kazi zake mikoa ya Shinyanga, Tabora na Singida ikijihusisha na mambo mbalimbali ikiwemo kupambana na ukatili wa kijinsia ametukiwa tuzo pamoja na cheti cha Ubingwa wa Mabadiliko kufuatia mafanikio makubwa ya taasisi hiyo.
Myola ametunikiwa tuzo hiyo na Taasisi ya Sheria na Maendeleo ya Wanawake WiLDAF-TZ katika mkutano uliofanyika Hoteli ya Protea Jijini Dar.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo mabalozi wa nchi mbalimbali, wasanii wa filamu, muziki, vikundi vya sanaa na wageni waalikwa kutoka mikoa mbalimbali.
Katika hafla hiyo mgeni rasmi alikuwa Balozi Getrude Mongella ambaye naye aliiasa jamii kutoendelea kufanya vitendo vya ukatili.
Akizungumza na mwanahabari wetu baada ya kutunukiwa tuzo hiyo, Myola alisema anaishukuru WiLDAF-TZ kwa kuuona mchango wa taasisi yake ambayo siku zote imekuwa ikifanyakazi bila kujua kama kuna siku mchango wao ungeweza kuonekana kwa kiwango hicho.
“Taasisi Agape yenye makao yake makuu mkoani Shinyanga imekuwa ikifanyakazi pamoja na mikoa ya Tabora na Singida ambapo tumekuwa tukifanyakazi mbalimbali ikiwemo kupambana na ukatili wa kijinsia.

“Miongoni mwa majukumu yetu ni kupambana na tatizo la mabinti wanaoachishwa shule kwa ajili ya kupewa ujauzito, kuolewa na umri mdogo, kufanyishwa kazi majumbani, mashambani na sehemu nyingine.
“Jambo lingine ni kuwasaidia kinamama wanaonyanyaswa katika ndoa zao.
“Baadhi ya misaada tunayowapa watoto wa kike ni pamoja na kuwaendeleza kielimu mabinti waliofeli shule za msingi na kuwasaidia kuendelea na masomo ya sekondari ya vyuo vya ufundi.
“Sisi wenyewe tuna kituo chetu kiitwacho Agape Training Centre ambacho kimekuwa kikitoa mafunzo mbalimbali kwa mabinti hao kama vile kutengeneza keki, kukausha mboga za majani, ushonaji na mambo mengine mengi.

Yote hayo tuliyafanya bila kujua kama ipo siku mchango wetu ungetambulika na kupewa tuzo kwenye hadhara kama hii” alisema Myola na kuishukuru WiLDAF-TZ. HABARI/PICHA ZOTE NA RICHARD BUKOS /GPL