
MBONGO Fleva mwenye uwezo wa juu, Omari Nyembo a.k.a Ommy Dimpoz amefunga mwaka vizuri baada ya kusaini mkataba na kampuni ya muziki, Sony Music Entertainment Africa ya jijini Johannesburg, nchini Afrika Kusini.
Akizungumzia mkabata huo mpya na Dimpoz, Mkurugenzi Mtendaji wa Sony Music Entertainment Africa, Sean Watson anasema: “Tunajivunia sana kuwa na msanii wa kiwango cha Ommy Dimpoz, tumefurahi sana Ommy kufanya uamuzi wa kushirikiana nasi – Sony. Tunafurahi kuungana naye kuleta muziki wake mzuri na wa kushangaza masikioni mwa mashabiki wengi kadiri tuwezavyo.”
Dimpoz alithibitisha kujiunga na kampuni hiyo, ambapo pia alitangaza rasmi kuwa wimbo wake wa kwanza ‘Dede’ kutoka kwenye album yake ijayo umeshatoka rasmi tangu juzi Desemba 10, mwaka huu.
Wimbo huo mpya kutoka kwa Ommy Dimpoz, umewashirikisha Dj Tira, Dladla Mshunqisi na Prince Bulo.
“Nimefurahi kujiunga na Sony, nyumba ya wasanii wenye vipaji duniani, ushirikiano huu ni hatua muhimu sana kwenye muziki wangu na umekuja wakati sahihi kwenye maisha yangu,” anasema Dimpoz akizungumzia kujiunga na kampuni hiyo.
Aidha, katika hatua nyingine, Dimpoz aliweka wazi kuwa album yake hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa itatoka rasmi mapema mwakani, ikiwa chini ya ushirikiano wake na Kampuni ya Sony Music Entertainment Africa.
Itakumbukwa kuwa Ommy alianza muziki kama mwimbaji wa bendi ya msanii wa Kibongo, Khaleed Mohamed T.I.D kabla ya baadaye kuibuka kama mwanamuziki wa kujitegemea na wimbo wake wa kwanza ukawa ni ‘Nai Nai’ akiwa amepiga kolabo na Alikiba.T.I.D ni kama alimfungulia milango ya muziki, kwani baadaye alitoka na kibao ‘Mama’ akiwa ameshirikiana na msanii mkali wa Bongo Dansi, Christian Bella.‘Me and You’ wimbo alioshirikiana na msanii Vanessa Mdee ukamtambulisha ndani ya mipaka ya Afrika Mashariki na hapo ndipo Ommy alipoendelea kuwasha moto kwenye ulimwengu wa muziki.
Vibao vyake vingine ni pamoja na Hello Baby aliomshirikisha msanii Avril kutoka Kenya, Achia Body, Tupogo, Wanjera, Ndagushima na Kajiandae.