
MBEYA: Taharuki imetanda baada ya mfanyabiashara Justin Justin (30), mkazi wa Upangwa wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe kulazimika kukimbilia kusikojulikana baada ya kudaiwa kumuua mfanyabiashara mwenzake aliyetajwa kwa jina moja la Peter.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwa, baada ya mauaji hayo, aliutia mwili wa Peter kwenye kiroba salfeti kisha kumzika.
Baada ya hapo, inasemekana kwamba alibeba pesa na bidhaa zote zilizokuwa dukani kwa marehemu na kuhamishia dukani kwake.
Tukio hilo la aina yake lilijiri hivi karibuni katika Kijiji cha Mahenge Kata ya Mpunguti wilayani Kyela Mkoa wa Mbeya.
Justin anadaiwa alikuwa akiuza duka lake katika Kitongoji cha Mbyaso na baada ya kuona biashara inamuendea vizuri alisafiri kwenda kijijini kwao, Upangwa-Ludewa ambapo alimshawishi Peter aende kuweka kioski kijijini alipoweka yeye duka ambapo kijana huyo alikubali hivyo waliondoka wote kwa ajili ya kwenda kufanya biashara.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mahenge, Asangalwisye Mwampondele alilieleza UWAZI kuwa, tukio hilo lilijiri usiku ambapo watu waliona godoro likiwa kitongoji jirani na baadaye wakamuona Justin akibeba vitu kutoka kwenye kibanda cha mwenzake huyo na kuhamishia dukani kwake.
Alisema kuwa, baadaye Justin alionekana akichimba udongo eneo lingine na kufukia kitu eneo lingine na alipoulizwa anazika nini, alisema anamchimbia kisima cha maji cha rafiki yake huyo ambaye amekwenda kijijini kusalimia.
Baada ya kuwepo kwa shaka juu ya kitu alichokuwa akizika Justin, mwenyekiti wa kijiji alitoa taarifa kwa viongozi wengine ili uchunguzi ufanyike kwani aliingiwa na wasiwasi.
“Baadaye mwenyekiti alifika akiwa na ofisa mtendaji kisha safari ya kwenda kwa Justin ikaanza,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mahenge, Simon Kalambo alisema walifika nyumbani kwa mtuhumiwa na kumhoji kuhusu alipo rafiki yake, akasema alikwenda nyumbani Ludewa kusalimia.
Alisema baada ya kutoa jibu hilo aliingia ndani kwake kisha alitokea mlango wa uani na kutoweka kijijini hapo.
Alisema kuwa, baada hapo walipiga simu Polisi ambao walifika na kuonesha eneo la tukio.
Alisema Polisi walimpigia simu daktari wa Serikali ambaye alifika akiwa na wasaidizi wake waliovalia glovu baada ya kuhisi katika eneo lililokuwa likifukiwa na Justini kulikuwa na mtu.
Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Kain Mwampempe alisema tukio hilo limewashangaza wengi na kuongeza kuwa ni la kwanza kutokea kwenye kijiji hicho.
Alisema kuwa, awali, Justin alifika kijijini hapo kama machinga na baadaye alifungua duka dogo na baadaye alikwenda kwao na kurejea na Peter ili naye aje kufanya biashara katika kijiji hicho.
Alisema kuwa, baada ya Peter kuweka duka kijijini hapo, biashara ilimuendea vizuri kwani alikuwa na wateja wengi ambapo alionekana kumzidi mwenzake aliyemleta kijijini hapo.
Alisema Polisi na madaktari walifukua eneo hilo na kukuta mwili wa kijana huyo ukiwa umefungwa kwenye kiroba ndipo walipofanya uchunguzi wa kitabibu.
Alisema kuwa, baada ya uchunguzi walibaini kuwa mwili huo ulikuwa umeanza kuharibika ndipo ikabidi wauzike eneo hilohilo chini ya usimamizi wa Serikali.
Aliendelea kusema kuwa, Polisi waliondoka na mke wa mtuhumiwa na rafiki yao ambapo wote wanashikiliwa kwenye Kituo cha Polisi cha Kyela.
Aliongeza kuwa, baada ya hapo, taarifa zilifika kwa ndugu wa marehemu ambapo kesho yake walifika na kutoa taarifa Polisi na Serikali wakihitaji kuufukua mwili huo ili waende kuuzika kijijini kwao.
Alisema Serikali iliwaruhusu wakafukua na kuondoka na mwili huku wakijisemesha kuwa waliohusika na tukio hilo watakiona.
Nao majirani waliozungumza na UWAZI akiwamo Lwitiko Mwabulanga walisema kuwa, Justin alipoona anazidiwa kipato na mwenzake ambaye kesho yake ilikuwa aende mjini kufunga mzigo, mtuhumiwa alimpa ofa ya pombe alipomsindikiza hadi kibandani kisha kutekeleza mauaji hayo kwa kumpiga na kitu chenye ncha kali kichwani kisha alimtia kwenye kiroba na kwenda kumzika jirani na kibanda chake.
Taarifa za Kipolisi zilieleza kuwa, bado mtuhumiwa anasakwa na Polisi ili sheria ichukue mkondo wake.
HABARI; Ibrahim Yassin, Uwazi