×

Mwanamke Asakwa Akituhumiwa Kufanya Mapenzi ya Jinsia Moja na Watoto

PEMBA: Mwanamke mmoja Salma Mohamed Hamed ameshtakiwa polisi kwa tuhuma za kushiriki mapenzi ya jinsia moja na watoto wa shule za sekondari na wasichana wenye zaidi ya miaka 18 kisiwani Pemba.

 

Mtuhumiwa huyo tayari ameripotiwa polisi na wazazi wa watoto waathirika kwa madai ya kudhalilishwa kingono, kosa ambalo ni kinyume cha utamaduni wa nchi na ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

 

Mmoja wa wazazi wa mabinti waliompelekea mtuhumiwa polisi, Mwajuma Omari alidai mtuhumiwa huyo aliwalaghai watoto wao kwa kuwapa zawadi na fedha na kuwafanyia vitendo hivyo; jambo ambalo ni hatari kwa jamii.

 

“Mmoja wa watoto hao alitoa siri hiyo kwangu. Kwa kweli tumechukizwa na tabia ya mama huyo na tumemshtaki polisi ili sheria ichukue mkondo wake.

 

“Mbaya zaidi ni kwamba huyu mama tunajua kwamba ametoroka nyumbani kwake na inasemekena yupo nje ya nchi.

“Ametoroka kwa sababu watu walikuwa na hasira na amejua kwamba wangeweza kumfanyia kitu mbaya kwa sababu wazazi ambao watoto wao walitoa ushuhuda kupandwa na hasira.

 

“Jambo la msingi ambalo nawaambia wazazi wenzangu ni kwamba wanatakiwa kuchunga watoto wetu,” alisema Rauhia Mussa; mmoja wa wazazi wa watoto waliodaiwa kufanyiwa vitendo hivyo.

 

Ofisa Polisi mmoja wa Kituo cha Polisi Konde amekiri kupokea malalamiko ya wazazi hao na kusema mtuhumiwa Salma Mohamed Hamed ametoroka na hajulikani alipo.

 

“Inawezekana ametoroka kwa sababu inasemekana kuna wazazi wamemtishia maisha, hivyo akaamua atokomee kusikojulikana,” alisema Ofisa polisi huyo akiomba kutoandikwa jina lake gazetini kwa kuwa sio msemaji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Ahmed Makaran hakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia tukio hilo.

 

Vitendo vya aina udhalilishaji kingono vimekuwa vikitokea sehemu mbalimbali visiwani Pemba ambapo pia baadhi ya wanaume huchukua watoto wa kiume na kuwadhalilisha kingono, jambo ambalo polisi wamekuwa wakilivalia njuga na kuwakamata watuhumiwa kisha kuwafikisha mahakamani na wengine kujikuta wakifungwa jela.

HABARI; Mwandishi Wetu, Uwazi

Leave a Comment