×

Tuisila Ashusha Presha Yanga, Kuwavaa Dodoma Jiji

HABARI njema kwa mashabiki wa Yanga ni kuwa kiungo wao kipenzi Mkongomani Tuisila Kisinda yupo fiti baada ya kupatiwa matibabu na upo uwezekano wa kuwa kwenye sehemu ya kikosi kitakachowavaa Dodoma Jiji FC.

 

Kiungo huyo juzi alishindwa kumalizia mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mwadui FC baada ya kupata majeraha ya goti yaliyosababisha ashindwe kuendelea na mchezo huo.

 

Yanga katika mchezo huo walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 5-0 kati ya hayo moja lilifungwe yeye Tuisila kwa shuti kabla ya kuumia na kutolewa nje kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Akizungumza na Championi Jumatano, Daktari Mkuu wa timu hiyo, Shecky Mgazija alisema kuwa mashabiki wa Yanga wasiwe na hofu, kwani mchezaji wao Tuisila yupo fiti kwa ajili ya mchezo ujao wa ligi dhidi ya Dodoma Jiji.“Ninafahamu mashabiki wengi wa Yanga wanataka kufahamu maendeleo ya Tuisila, kwa kifupi ni kuwa anaendelea vizuri baada ya kumpatia matibabu ya haraka pale uwanjani.

 

“Majaraha yenyewe aliyoyapata siyo makubwa sana, zaidi alipata mshtuko kwenye sehemu ya goti, hivi sasa anaendelea vizuri baada ya matibabu ya haraka tuliyompatia.

 

“Hivyo, huenda akawa sehemu ya kikosi kitakachocheza na Dodoma Jiji katika mchezo wa ligi wiki hii, hivyo mashabiki waondoe hofu kwenye hilo mchezaji wao yupo fiti kabisa,” alisema Mgazija

STORI NA WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave a Comment