
INATAJWA kuwa ugonjwa wa kupooza mwili ambao ulikuwa ukimsumbua muigizaji nguli nchini Tanzania, Mohamed Fungafunga, maarufu kama Jengua ndiyo sababu iliyopelekea kifo cha mzee huyo aliyefariki jana Jumanne akiwa kwa mwanaye Mkuranga, Pwani.
Msanii mwenzake, Blandina Chagula ‘Johari’, amethibitisha kufariki kwa msanii huyo na kueleza kwamba alikuwa akiugua kwa muda mrefu baada ya kupooza na kwamba mauti yalimkuta akiwa anaendelea na matibabu.”
Ni kweli tumepewa taarifa za kifo chake, alikuwa anapatiwa matibabu Mkuranga kwa mwanaye, kwa muda mrefu sana alikuwa anasumbuliwa na stroke,” alisema Johari.
Lakini kwa upande wa Chama cha Waigizaji Dar es salaam TDFAA, kupitia kwa Katibu Mkuu, Doricy Kante alithibitisha pia kutokea kwa kifo hicho na kuweka wazi kuwa taratibu za mazishi yake zitatolewa wakati wowote.
Mzee Jengua alipata umaarufu mkubwa katika mchezo wa runinga wa Kidedea uliokuwa ukirushwa na Kituo cha ITV na kutayarishwa na Chemchem Arts Group, akiigiza kama mzee katili na mwenye roho mbaya.
Enzi za uhai wake, Jengua aliigiza maigizo kama vile Kidedea, Handsome wa Kijiji, Kashinde na zingine nyingi.
Issa Liponda,Dar es Salaam