×

Wawekezaji Wamiminika FHF, Hati Fungani Yavuka Lengo Kwa Mara 6

Hati Fungani ya Makazi iliyotolewa na First Housing Finance (FHF) Tanzania na kuratibiwa na Stanbic Bank Tanzania imepata usajili wa ziada wa asilimia 661, jambo linaloashiria imani kubwa ya wawekezaji katika sekta ya mikopo ya nyumba nchini pamoja na kuongezeka kwa uaminifu katika bidhaa za uwekezaji kupitia masoko ya mitaji.

Hati hiyo ilivutia uwekezaji wenye thamani ya shilingi bilioni 33.08, kiwango kilichozidi kwa mbali lengo la awali la kukusanya shilingi bilioni 5.0. Mafanikio haya yanaonyesha hamasa kubwa ya wawekezaji kwa bidhaa bunifu za kifedha na kusisitiza nafasi muhimu ya masoko ya mitaji katika kukusanya fedha za muda mrefu kwa ajili ya maendeleo.

Mwitikio huo mkubwa unaiweka Hati Fungani ya Makazi miongoni mwa hati fungani zilizofanya vizuri zaidi katika historia ya hivi karibuni ya utoaji wa hati fungani za shilingi za Tanzania, huku ikiakisi ukuaji na uimara unaoendelea wa masoko ya mitaji nchini.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa FHF Tanzania, Bw. Charles Mugila, alisema mafanikio hayo ni hatua muhimu kwa taasisi hiyo na kwa sekta nzima ya fedha nchini.

“Ufanisi huu unaonyesha kiwango kikubwa cha imani ambacho wawekezaji wanacho kwa taasisi yetu pamoja na ukuaji unaoendelea wa masoko ya mitaji nchini Tanzania. Kama Bodi, tumejizatiti kuhakikisha fedha hizi zinatumika kwa umakini, uwazi na ufanisi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa,” alisema.

Kutokana na mahitaji makubwa ya wawekezaji, kampuni ilipata kibali kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Tanzania (CMSA) kukubali shilingi bilioni 28.15 ili kusaidia kupanua huduma za mikopo ya nyumba nchini kote.

Afisa Mtendaji Mkuu wa First Housing Finance (FHF), Amulike Kamwela (kulia) akizungumza na Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji Stanbic Bank, Sarah Mkiramweni (kushoto), wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa Makazi Bond katika soko la hisa la Dar es Salaam Jumanne. Katikati ni Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Mary Mniwasa.

Kuorodheshwa kwa Hati Fungani ya Makazi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) tarehe 9 Juni 2026 kumeongeza thamani ya uwekezaji katika hati fungani za kampuni kwa asilimia 1.63 hadi kufikia shilingi trilioni 2.06 kutoka trilioni 2.03, hatua iliyochangia kuimarisha zaidi soko la mitaji la Tanzania.

Mafanikio ya usajili huo yanatarajiwa kuongeza uwezo wa FHF kutoa suluhisho za kifedha za umiliki wa nyumba kwa Watanzania wengi zaidi, hivyo kuunga mkono juhudi za taifa za kupanua upatikanaji wa makazi nafuu na kuchochea ukuaji wa sekta za ujenzi na biashara ya majengo.

Mtendaji Mkuu wa CMSA, CPA Nicodemus Mkama, alisema mafanikio ya hati fungani hiyo yanaonyesha kuongezeka kwa imani ya wawekezaji kwa First Housing Finance pamoja na masoko ya mitaji ya Tanzania kwa ujumla.

Kwa mujibu wa CMSA, wawekezaji binafsi walichangia asilimia 96.63 ya jumla ya usajili, huku wawekezaji wa taasisi wakichangia asilimia 3.37, jambo linaloonyesha kuongezeka kwa ushiriki wa Watanzania wa kawaida katika uwekezaji kupitia masoko ya mitaji.

CPA Mkama alieleza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na mazingira bora ya kisera, kisheria na kiutendaji yaliyowekwa na Serikali kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji kupitia masoko ya mitaji.

“Mafanikio haya yamewezeshwa na motisha mbalimbali, ikiwemo kuondolewa kwa kodi ya zuio kwenye mapato yatokanayo na hati fungani za kampuni, hatua iliyofanya bidhaa hizi za uwekezaji kuwa kivutio zaidi kwa wawekezaji,” alisema.

Aliongeza kuwa utoaji huo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha, unaolenga kuboresha upatikanaji wa fedha za muda mrefu kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta za umma na binafsi.

Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji Benki wa Stanbic Bank Tanzania, Bi. Sarah Mkiramweni, alisema usajili huo mkubwa pamoja na kuorodheshwa kwa Hati Fungani ya Makazi unaimarisha zaidi nafasi ya Tanzania kama moja ya masoko yanayoongoza ya mitaji katika Afrika Mashariki.

Alisema Stanbic inajivunia kuwa mratibu mkuu wa shughuli hiyo, ikifanya kazi kwa karibu na washauri wengine pamoja na wadhibiti wa sekta hiyo, wakiwemo CMSA, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na DSE, kuhakikisha hati fungani hiyo inafanikiwa kuingia sokoni.

“Masoko ya mitaji yanaendelea kuwa chanzo muhimu cha upatikanaji wa fedha kwa taasisi mbalimbali, na Stanbic itaendelea kusaidia mashirika yanayotafuta mbinu mbadala za ufadhili kupitia utoaji wa hati fungani na zana nyingine za kifedha,” alisema Bi. Mkiramweni.

Aliongeza kuwa Tanzania inanufaika na mfumo imara wa udhibiti pamoja na uwepo wa kundi tofauti la wawekezaji, likijumuisha taasisi, wawekezaji binafsi na taasisi za kimataifa za maendeleo ya kifedha, hali inayochangia mafanikio ya utoaji wa hati fungani nchini.

Akizungumzia sekta ya makazi, Bi. Mkiramweni alisema Stanbic itaendelea kuunga mkono ajenda ya Serikali ya maendeleo ya makazi kupitia mikopo ya nyumba na kusaidia taasisi za fedha za makazi kupata mitaji nafuu kwa ajili ya utoaji wa mikopo.

“Maendeleo ya makazi ni sehemu muhimu ya matarajio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Kama moja ya benki zinazoongoza nchini, tumejipanga kuendelea kusaidia suluhisho za ufadhili wa muda mrefu zinazoongeza umiliki wa nyumba na kuchochea ukuaji wa uchumi,” alisema.

Wachambuzi wa masoko wanaamini kuwa mafanikio ya Hati Fungani ya Makazi yatahamasisha taasisi nyingi zaidi zisizo za kibenki kutumia masoko ya mitaji kupata fedha, jambo litakalopanua chaguzi za ufadhili kwa biashara mbalimbali huku likiimarisha ushiriki wa wawekezaji na maendeleo ya soko kwa ujumla.

Leave a Comment