×

Niliolewa na Mganga kwa Tamaa ya cheo

ILIPOISHIA:

“Vipi shoga unaonekana leo una furaha kulikoni?”

“Mh! Mbona makubwa madogo yana nafuu.”

“Yepi tena hayo shoga?”

“Kwa vile tunakwenda pamoja nisikuonjeshe ukakinahi mapema.”

Sikutaka kuongeza neno nilibeba begi langu na kuongozana na Safi kuelekea kwenye gari langu.

SASA ENDELEA…

Baada ya kuingia ndani ya gari tuliondoka eneo la kazini huku nikiwa na hamu ya kujua ubuyu huo una ladha ya aina gani.

Tulipotoka kidogo Safia alianza kunipa ubuyu nami nilitega masikio huku mapigo ya moyo yakinienda mbio.

“Basi dada kuna bonge la gogoro.”

“Lipi tena hilo?”

“Aliyeteuliwa kagoma kwenda mpaka aipate ndoa.”

“Mteuliwa nani?”

“Si Happy.”

“Happy yupi?”

“Aliyewaengua na kuchaguliwa kwenda kusoma ili akirudi awe juu yenu.”

“Mh!”

“Basi ndiyo kagoma kasema haendi mpaka wafunge ndoa anataka aondoke kama mke wa mtu na si mchumba.”

“Sasa kuna tatizo gani bado muda upo wa kufunga ndoa na kwenda kusoma.”

“Kweli walikuwa na mpango wa kufunga ndoa lakini safari ya kwenda kusoma ilivuruga kila kitu.”

“Kama walikuwa wameshajipanga wanaweza kwenda kufunga ndoa tu sherehe akirudi.”

“Inavyosemekana walikubaliana kufunga ndoa baada ya kurudi, lakini kuna taarifa kazipata kuwa mchumba wake ana mwanamke mwingine kitendo cha kwenda kusoma huku nyuma wanafunga ndoa na akirudi akute kila kitu kimekwisha.”

“Mh! Makubwa, sasa yeye taarifa hizo kazitoa wapi?”

“Hata najua.”

“Wewe nani kakuambia?”

“Mkurugenzi.”

“Ilikuwaje mpaka akakueleza habari hizo?”

“Huwezi kuamini leo meneja alikuja mapema na kuingia kwa mkurugenzi, wamekaa ndani zaidi ya saa nne. Alipotoka alionekana kachanganyikiwa, si ndiyo mama usipitwe nikamfuata mkurugenzi kutaka kujua kuna kitu gani kimemtokea meneja.

“Ndipo aliponipa ubuyu huu, kuna kitu alinieleza kuwa kama itashindikana wangemteua mtu mwingine haraka kabla ya Jumatano si ndiyo na mimi nikapiga chapuo uende wewe.”

“Ehe! Akasemaje?”

“Akasema anasubiri jibu la meneja atakalompa jioni kuwa mchumba wake anakwenda au haendi. Kama haendi kesho asubuhi waanze mchakato wa kumtafutia viza mtu watakayemteua.”

“Mh!” Nilijikuta nikiguna tu.

“Tena huwezi kuamini maombi yangu yule msichana akatae kwenda ili uende shoga yangu.”

“Bado muda huenda wakakubaliana.”

“Aah, wapi mwanamke yule ameapa hatakwenda bila ndoa.”

“Mh! Ngoja tuone.”

“Ukweli wa mbivu na mbichi utazijua kesho asubuhi.”

Nilimpeleka Safia mpaka kwake kisha nilirudi nyumbani kupumzika nilijiuliza yaliyozungumzwa na Safia yana ukweli gani. Nilijikuta nikitabasamu mwenyewe baada ya kuiona kauli ya babu inakaribia kuwa kweli. Niliamini jibu la kesho ndilo litanipa picha kamili kama nitakwenda mimi au la!

Wasiwasi wangu ilikuwa kama kitaitishwa kikao cha bodi ya uteuzi ningeweza kupoteza nafasi ile. Lakini majina niliyopeleka kwa babu niliamini yakafanya kazi japokuwa sikuwa na uhakika kama watakuwa ni walewale.

                                                   ***

Siku ya pili nilikwenda kazini kama kawaida nikiwa na shauku kutaka kujua kuna jipya gani kutokana na kauli ya mchumba wa meneja kama bado ana msimamo uleule wa kutaka ndoa kabla ya kwenda au kuna mabadiliko yoyote. Kama kawaida kabla ya kazi nilimpigia simu Safia kumjulia hali lakini nikiwa nataka kujua kuna habari gani mpya juu ya taarifa alizonipa jana yake.

Baada ya salamu hakuna kilichoendelea zaidi ya kunitakia kazi njema, nilijiuliza ina maana hakukuwa na kipya kutokana na taarifa zake za jana yake.

“Safia bosi amefika?” nilijifanya kumuulizia bosi ili nisikie Safia ana taarifa gani.

“Muda tu.”

“Vipi kuna jipya?”

“Mpaka sasa sijasikia kitu ndiyo maana sijakueleza chochote.”

“Kwani meneja leo hajaja?”

“Sijamuona.”

“Labda wamemalizana.”

“Kina nani?”

“Meneja na mchumba wake.”

“Mh! Kwa kweli nami bado nipo njia panda maana jana alinieleza jibu la kusafiri au kutosafiri ningelipata asubuhi lakini imekuwa kimya.”

“Kwani mkurugenzi anaonekanaje?”

“Yupo kawaida.”

“Mh! Sawa, hukumuuliza?”

“Nitaanzia wapi, siku zote mimi mtekelezaji kuuliza ni kiherehere labda alianzishe yeye ndipo nimchimbe.”

“Mh! Sawa.”

“Shoga usikate tamaa hata kama hutaenda bado thamani yako ni kubwa sana.”

“Basi baadaye.”

“Poa.”

Nilikata simu ili niendelee na kazi lakini hamu yote ilikatika hasa nilipokumbuka kauli ya Safia kuwa hata nikikosa sitapungukiwa na kitu bila kujua jinsi gani nilivyoitafuta nafasi hiyo kwa udi na uvumba kufikia hatua ya kujidhalilisha kwa kiasi kikubwa. Kwa kauli ile ilionesha wazi hakukuwa na safari.

Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake katika Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Leave a Comment