
WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, ameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa maji wa Mzakwe wenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 200 unaotarajiwa kupunguza adha ya maji kwa Mkoa wa Dodoma huku akimuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuhakikisha vinachimbwa visima vingine vikubwa viwili.
Ameyasema hayo usiku wa Disemba 20, 2020, wakati akizungumza na waandishi wa habari alipofanya ziara ya kushtukiza kukagua utekelezaji wa mradi wa maji wa Mzakwe ambapo amesema wizara imeipatia sh. bilioni moja Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kutatua changamoto hiyo.
Ameongza kwamba adha ya maji imetokana na kuwepo kwa ongezeko kubwa la watu akisema kuwauhitaji wa maji mkoa wa Dodoma ni lita milioni 103 wakati uzalishaji wa sasa ni lita milioni 66, ikionyesha upungufu wa lita milioni 37 huku akibainisha kuwa kisima hicho kinatarajiwa kuzalisha lita laki nne kwa saa.
Pia, ametoa onyo kwa baadhi ya watu wanaofanya mgao wa maji bila kufuata utaratibu akisema wizara haitomvumilia yeyote anatakayebainika kufanya ubabaishaji kwani serikali imejipanga kufanya kazi usiku na mchana kufikisha kwa kila Mtanzania huduma hiyo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji DUWASA, Mhandisi, Aaron Joseph, amesema mradi huo unafanywa na Kampuni ya Shanxi akieleza kuwa kisima kitakuwa na urefu wa mita 150 ambapo hadi sasa kimefikia theluthi ya utekelezaji wake. Mradi huo ulitarajiwa kukamilika ndani ya siku 60 lakini alisema watatekeleza kwa muda wa siku 30.
Aidha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi, Anthony Sanga, ameahidi kutekeleza maagizo yaliyotolewa huku akiwahimiza Watanzania kuendelea kutunza vyanzo vya maji katika maeneo yao.