
WANANCHI wa Kijiji cha Kanyara, Halmashauri ya Buchosa wametoa malalamiko yao kwa Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Mhe. Eric Shigongo, kuhusu kutozwa fedha nyingi kwenye Bandari ya Kanyara, ambapo wameibua madudu ya risiti za kuandika kwa mikono zinazotumiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) katika bandari hiyo badala ya risiti za kielektroniki.
Tukio hilo limejiri wakati wa mkutano na wananchi wa kijiji hicho juzi ambapo walimkabidhi Mhe. Shigongo risiti hizo za kuandika kwa mkono wanazopewa baada kulipa, huku wakidai kuwa hazionyeshi nani ameziandika na baadhi ya risiti hizo zimeandikwa Tanga wakati wao ni Mkoa wa Mwanza.
Hii imetokana na wananchi kuchoshwa na watendaji wa mamlaka hiyo Bandari ya Kanyara kwa kuwatoza kiasi cha Tsh. 600 wanapoingia kwenye eneo la bandari hiyo kabla ya kulipia nauli ya boti kiasi cha Tsh. 1,500 ili wavuke kwenda visiwani kwenye shughuli zao mbalimbali.
Aidha, wananchi hao wamedai kuchoshwa na manyanyaso ya baadhi ya watumishi wa bandari hiyo ambao wamedai kuwa wamekuwa wakiwapiga na kuwadharirisha huku wakiwatupia maneno makali.
“Mhe. Mbunge sisi tumechoshwa na manyanyaso ya watumishi wa Bandari, tunapigwa, tunatukanwa, tunaambiwa hatutambuliki hapa, tozo ni kubwa tunaomba ipunguzwe. Hata tukilipa pesa tunapewa risiti za mkono badala ya EFD, jambo ambalo si sawa, tunaomba kero yetu uishughulikie.
Akijibu kero hiyo, Mhe. Shigongo amesema tayari ameshaanza kulifanyia kazi jambo hilo kwa kushirikiana na wahusika (TPA) huku akiahidi kuweka rehani ubunge wake iwapo suala hilo halitaisha.
“Nipo radhi kwenda kulala kwenye mlango wa Ikulu ili nimweleze Mhe. Rais, haiwezekani wananchi wetu wanyanyaswa. Nitaweka rehani ubunge wangu kuhakikisha tozo hiyo inapungua. Mhe. Rais ameshaagiza na kusisitiza mara kwa mara kuhusu risiti za EFD lakini bado kuna watu hawajamuelewa, hatupo tayari kupoteza mapato sababu ya watu wachache,” amesema Shigongo.