
MAMBO mazito yanazungumzwa juu ya kifo cha ghafla cha Bilionea Igor Sosin (53), raia wa Urusi aliyekutwa amekufa hotelini visiwani Zanzibar, alikokwenda kwa mapumziko akiwa ameambatana na binti yake, Taisia (18), UWAZI limechimba.
Hiyo ndiyo habari nzito iliyoshtua wengi Bongo katika msimu huu wa Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.
Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi visiwani Zanzibar, ACP Awadh Juma Haji alisema kuwa, Sosin alikutwa amefariki dunia usiku wa Desemba 23, 2020 katika chumba cha Hoteli ya Park Hyatt iliyopo Mtaa wa Mji Mkongwe mjini Unguja.
MAZINGIRA YA KIFO CHA SOSIN
Mazingira ya kifo chake yamejawa kugubikwa na utata mzito, kwani inaelezwa kuwa, katika chumba alimofia, Sosin hakuwa peke yake. Alikuwa na mwanamke wa Kitanzania, Arafa Ramadhan Mpondo (23), mkazi wa Fuoni Zanzibar ambaye inaelezwa kwamba alikuwa na uhusiano naye wa kimapenzi baada ya kufahamiana naye mtandaoni.
Kwa maelezo ya Arafa, inadaiwa kuwa, siku ya tukio, muda wa saa 5:45 usiku, aligundua kwamba Sosin hakuwa vizuri kiafya, lakini akaamua kulala naye mpaka asubuhi ili taratibu za matibabu zianze, lakini kulipopambazuka, alijaribu kumuamsha bila mafanikio, alipoona haamki ndipo akatoa taarifa kwa uongozi wa hoteli na hapo ndipo ilipobainika kwamba alishafariki dunia.
Kamanda Awadh alieleza kwamba, mwili wa marehemu ulipelekwa Hospitali ya Mnazi- Mmoja kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ambapo majibu ya awali ya uchunguzi wa kidaktari, yalionesha kwamba bilionea huyo alikufa kifo cha kawaida, lakini bado uchunguzi wa kina unaendelea kufanyika, huku Arafa akiendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi.
Msemaji wa Hospitali ya Mnazi- Mmoja, Hassan Mcha Makame, alisema mwili wa marehemu ulitolewa damu kwa uchunguzi wa kimaabara kisha mwili huo ulikabidhiwa kwa familia yake kisha kusafirishwa kwenda nchini Urusi.
AUGUA, APONA CORONA
Gazeti la Daily Mail la Uingereza liliripoti kuhusu kifo cha bilionea huyo likieleza kuwa, mapema mwaka huu aliugua na kupona Ugonjwa wa Corona na alipanga kusherehekea Mwaka Mpya akiwa visiwani Zanzibar.
BILIONEA SOSIN NI NANI?
Igor Sosin ni bilionea wa Urusi anayeaminika kuwa na utajiri unaokadiriwa kuwa Dola za Kimarekani bilioni 18 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 41.5 za Kitanzania.
Kabla ya kuingia kwenye biashara zilizompatia utajiri mkubwa hasa baada ya kuanguka kwa mfumo wa kijamaa nchini Urusi, Sosin alikuwa mkandarasi wa mashine za ujenzi katika kampuni moja kubwa jijini Moscow, Urusi.
Baadaye aliamua kuachana na kazi hiyo na kujikita rasmi kwenye biashara za viwanda, akimiliki viwanda mbalimbali kuanzia vya kutengeneza nguo za bei rahisi, vifaa vya ujenzi, vinywaji mpaka uuzaji wa majumba na mashamba; yaani Real Estate.
Miongoni mwa biashara zake kubwa, ni umiliki wa Kampuni ya New Idea Investment Group ambayo inashughulika na uuzaji wa bidhaa mbalimbali za majumbani, lakini pia akiwa mjumbe wa bosi ya kampuni nyingine ya Structure Enterprises NV ambayo inashughulika na uuzaji wa vinywaji visivyo na kileo vya ZEO nchini Uingereza.
Pia alikuwa mmiliki wa Kampuni ya Cvetochny Standart LLC ambayo inamiliki msururu wa mahoteli ya Sarafina yaliyosambaa maeneo mbalimbali barani Ulaya, sambamba na kumiliki supermarket kadhaa barani Ulaya za OBI hypermarkets.
Inazidi kuelezwa kwamba makampuni mengine yaliyompatia utajiri mkubwa zaidi ni Starik Hottabych na Modi ambayo huuza nguo za kisasa kwa bei nafuu barani Ulaya.
MISUKOSUKO YA KIFAMILIA
Licha ya utajiri mkubwa aliokuwa nao, vyanzo mbalimbali vinaonesha kwamba maisha ya bilionea Sosin yalitawaliwa na misukosuko ya hapa na pale, kubwa likiwa ni tukio la mwaka 2015 ambapo mtoto wake, Egor Igor Sosin ambaye kwa kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 19, alimuua mama yake ambaye alikuwa mke wa pili wa bilionea huyo, Anastasia kwa kumkaba na waya wa chaja ya simu shingoni.
Tukio hilo lililotokea katika Hoteli ya Kazan lilizua gumzo la aina yake ambapo mtoto huyo alikamatwa na Polisi kwa kosa la mauaji na alipohojiwa, alikiri kumuua mama yake huyo kwa kile alichokieleza kuwa ilikuwa ni kumtoa mapepo ili akapumzike.
Baadaye ilibainika kwamba mtoto huyo alikuwa matatizo makubwa ya kiakili wakati akitekeleza mauaji hayo, akaachiwa huru na kupelekwa kwenye hospitali ya wagonjwa wa akili alikotibiwa kwa kipindi kirefu mpaka alipopona na kurudi uraiani.
Kama hiyo haitoshi, mpaka anafikwa na umauti, Bilionea Sossin alikuwa kwenye mgogoro mkubwa na mkewe wa tatu na walikuwa kwenye mipango ya kupeana talaka.
Miezi michache iliyopita, bilionea huyo pia alipata maambukizi ya Virusi vya Corona, hali iliyosababisha apiganie uhai wake kwa zaidi ya miezi mitatu na baada ya kupona, alijiwekea nadhiri ya kwenda kula bata visiwani Zanzibar kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2021, kabla ya kufikwa na mauti.
MAISHA YA ANASA
Bilionea Sossin alipata umaarufu mkubwa kutokana na mfumo wake wa kuishi maisha ya kifahari au kula bata kupindukia. Inaelezwa kwamba, Sosin alikuwa akipenda sana kuzunguka Dunia nzima akiwa ndani ya boti yake ya kifahari yenye kila kitu, lakini pia alikuwa mpenzi wa mchezo wa tenisi na kuteleza kwenye barafu.
Wakati wa uhai wake, Sosin aliweka wazi kuwa anapenda kuishi maisha ya kifahari na starehe ilikuwa na nafasi kubwa kwenye maisha yake.
Mara kwa mara alikuwa akionekana katika Fukwe za Cote d’Azur au maarufu kama French Riviera akistarehe na kufanya pati zilizokuwa zinagharimu mamilioni ya pesa.
Kama hiyo haitoshi, bilionea huyo pia alikuwa na kawaida ya kusafiri hadi nchini Marekani na kukodi jumba la kifahari la Ox Pasture Lane lililopo Southampton, miongoni mwa majengo ya kifahari yaliyokuwa yakikodishwa kwa pesa nyingi, likiwa na kila kitu ndani. Akiwa humo, kazi yake ilikuwa moja tu, kuponda sterehe!
Huyo ndiye Igor Sossin, bilionea wa Urusi aliyefariki dunia akiwa anakula bata visiwani Zanzibar.
HABARI; MWANDISHI WETU NA MTANDAO