×

Jumbe Asimulia Alivyovunjwa Mguu na Kuku Ndotoni

UMEWAHI kusikia kisa cha mtu kuvunjwa mguu na kuku?

Leo ukiambiwa mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Hussein Jumbe amevunjika mguu baada ya kupambana na kuku akiwa ndotoni utaona ni maajabu ya mwaka 2020.

Siyo simulizi ya kutunga bali ni ya kweli ambapo mwanamuziki huyo alimwambia mwandishi wetu hivi karibuini kuwa yuko kwenye wakati mgumu baada ya kuvunjika mguu kimaajabu akiwa ndotoni.

MWANDISHI: Vipi kaka unaonekana ukiwa na P.OP mguuni ulipata ajali?

JUMBE: Aaah, majanga tu kaka haya.

MWANDISHI: Ya nini tena?

JUMBE: Ni kama mauzauza ya duniani ndugu yangu.

MWANDISHI: Unamaanisha mambo ya kishirikina ndiyo yamekuvunja mguu?

JUMBE: Jumamosi moja nikiwa nyumbani kwangu Temeke Mikoroshini niliota niko kijijini kwetu naendesha baiskeli sasa ghafla mbele yangu alitokea mtu na kunizibia njia.

MWANDISHI: Hapo ulikuwa unaota…ehee ikawaje sasa?

JUMBE: Nikamkwepa huyo aliyeniziba kwa kupita pembeni, lakini baada ya kumpita mbele yangu akatokea mtoto ananilenga na manati.

MWANDISHI: Ehee!

JUMBE: Naye nilimpita lakini baada ya kumpita akapiga jiwe kwa kutumia manati kwenye tairi la nyuma ya ile baiskeli yangu.

MWANDISHI: Duh!

JUMBE: Hapo nilipatwa na jazba na kugeuza baiskeli ili nikamuulize kwa nini aliamua kunifanyia vile, nilipomkaribia yule mtoto aligeuka kuku ndipo tukaanza kupambana.

MWANDISHI: Kupambana kwa maana ya kupigana na kuku?

JUMBE: Ndiyo nilianza kumshambuliwa kwa mateke.

MWANDISHI: Hatari sana…!

JUMBE: Mapambano yakiwa yamekolea ndipo mke wangu alishtuka usingizini na kuniamsha nikiwa nimelowa jasho chapachapa.

MWANDISHI: Ni kama kulikuwa na mpambao wa laivu.

JUMBE: Kabisa na kusema kweli nilikuwa nasikia maumivu ya mguu, asubuhi kulipokucha mguu wangu uliendelea kuuma ikabidi twende hospitali nilipigwa X-Ray na kuonekana nimevunjika vidole vinne vya mguu wa kulia.

MWANDISHI: Pole sana Jumbe hiki ni kisa cha kushangaza sana.

JUMBE: Yaani ni maajabu yangu ya mwaka na kusema kweli nimetunga hadi wimbo kuhusu tukio hilo.

MWANDISHI: Lakini unaendeleaje hadi sasa?

JUMBE: Hali ndiyo kama unavyoina ni mwendo wa kujikokota na kutembelea magongo.

MWANDISHI: Pole sana kaka.

JUMBE: Asante ndugu yangu.

Ingawa imeripotiwa kwenye vyombo vya habari kuhusu tukio la mwanamuziki huyo kuvunjika mguu ndotoni watu wengi wamekuwa wakishangazwa na tukio hilo.

Hata hivyo Godfrey Chale daktari maarufu jijini Dar es Salaam alipoulizwa kitaalamu juu ya hali ya mtu kufanya mapambano akiwa ndotoni na kufikia kiasi cha kujeruhiwa alisema:

“Hali hiyo hutokea na kitalaam inaitwa Sleepwalking ambapo mtu anaweza kuamka na kutembea au kufanya vitendo vingine huku akiwa usingizini.

“Anaweza kupigana akiwa amelala na tukio likaonekana kama halisi kumbe anayelifanya anakuwa kalala.

“Sasa kwa kisa ambacho unaniambia naweza kukielezea katika muktadha huo, huwenda mzee wetu alikuwa anaota lakini katika hali ya kupambana na huyo kuku basi ikatokea amepiga teke ukuta na kujikuta amevunjika mguu.

“Sidhani kama ni uchawi ni hali ambapo sayansi inatambua.”

Jumbe amewahi kufanya kazi katika bendi mbalimbali ikiwemo Msondo Ngoma na sasa anamiliki bendi yake inayotwa Tallent ambayo inaundwa na vijana wenye vipaji huku kiwanja chao cha nyumbani kikiwa ni Ukumbi wa Kisuma, Mwembe Yanga uliopo Temeke jijini Dar.

STORI | RICHARD BUKOS, RISASI

Leave a Comment