×

Tandabui Yafadhili Wataalamu wa Masomo ya Afya 480

VIJANA 480 wasiokuwa na uwezo wamepata ufadhili wa masomo katika fani mbalimbali katika Chuo cha Afya cha Tandabui kilichopo jijini Mwanza kati ya mwaka 2012 hadi 2020.

 

Akizungumza mapema leo Ijumaa, Januari 8, 2020, katika mahafali ya chuo hicho, Mkuu wa Chuo, Walace Keto amesema tangu chuo hicho kianzishwe mwaka 2012, wamekuwa wakiwasomesha vijana wanaotoka kwenye maisha duni ambao hawana uwezo wa kulipia gharama za masomo ikiwa ni kutoa mchango wa chuo hicho kwa jamii.

Aliongeza kuwa kwa mwaka huu pekee wametoa nafasi za masomo kwa wanafunzi 100 wasikokuwa na uwezo ili kusoma bure.

Keto ameongeza kuwa chuo hicho kimekuwa kikitoa elimu kwa kuzingatia ubora na kwamba wamekuwa wakipata ushirikiano mzuri kutoka serikalini.

 

Aidha, katika kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu bora, Keto ameiomba serikali kuwapatia huduma ya maji ya uhakika, kupatiwa ulinzi eneo la chuo pamoja na kujenga miundombinu ya barabara sambamba na kuwapatia fursa wanafunzi wao kupata hospitali za kufanyia mafunzo kwa njia ya vitendo.

Akizungumza baada ya kuwatunuku vyeti wanafunzi, 1935 kwa mwaka 2020, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza, Dk. Phiris Nyimbi ameahidi kutatua baadhi ya changamoto zinazokwamisha juhudi za utoaji elimu chuoni hapo, ikiwemo kuimarisha ulinzi pamoja na miundombinu.

Dk. Nyimbi amewataka wahitimu hao kutumia taaluma waliyopata kujiajiri na kuajiri vijana wengine. Fani waliohitimu ni pamoja na uuguzi, famasia, utabibu, maabara ya matibabu, utunzaji kumbukumbu za afya na afya ya jamii.

Na Leah Marco, MWANZA

Leave a Comment