×

Rais Nyusi: Magufuli Sili Sembe, Mama Nyerere Alinipikia Mbuzi – Video

RAIS wa Jamhuri ya Msumbiji, Filipe Jacinto Nyusi, amewasili Uwanja wa Chato Mkoa wa Geita katika ziara yake ya kikazi ya siku mbili hapa nchini kuanzia leo Jumatatu, Januari (11 -12, 2021) na kupokelewa na mwenyeji wake, Rais Dkt. John Magufuli.

 

Katika ziara hiyo,  Nyusi na  Magufuli wameweka jiwe la Msingi la Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Nyamilembe, wilayani Chato mkoani Geita.

Akizungumza wakati wa hafla ya mapokezi na uzinduzi huo,  Nyusi amesema: “Juzi nilimpigia simu Rais Magufuli nikamuuliza uko wapi, na mara nyingi tunaongea asubuhi mapema, akasema yupo Chato, nikamuuliza Chato ni wapi? Akasema Chato nyumbani kwetu, nikamwambia nakuja shule uliyosoma, akasema njoo, sili sembe nakula ugali wa kusaga, akasema nitakusagia.

 

“Nakupongeza Mhe. Rais kwa kuangalia maisha ya wananchi, hii hospitali haina chama ni ya wananchi, huu ni mkoa mpya wakati tunagombea ukombozi wa Msumbiji huu mkoa tulikuwa hatuujui, tulikuwa tunafahamu Mwanza kwa Wakerewe.

 

“Nakupongeza Rais Magufuli kwa kujenga Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato, Hospitali hii haina chama itatumiwa na wote, nashukuru kwa kunipa heshima ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali hii, nitakuwa napiga simu kila Jumamosi kuulizia ujenzi umefikia wapi.

 

 

“Nimeona hapa Chato ni karibu na Rwanda, Uganda na Kenya hivyo hii hospitali itawasaidia hata ndugu zetu hawa wasiende mbali. Rais Magufuli anashughulika sana juu ya maisha ya Watanzania, kutafuta nyumba nzuri za kukaa, chakula, maji na afya, na afya anayotaka ni ile ya quality.

 

“2014 nilifika hapa Tanzania, nilipokelewa na Mama Maria Nyerere, alinipikia mbuzi nyumbani kwake aliniusia utakuwa rais ndiyo, lakini usisahau lazima uwe na kiwanda kimoja tu cha dawa, watu wanakufa kwa kukosa tu dawa ya Aspirin.”

 

Kwa upande wake, Rais Magufuli amesema biashara kati ya Tanzania na Msumbiji imeongezeka hadi Sh. bilioni 93.6 mwaka 2020 ambapo Tanzania na Msumbiji ni ndugu na kuna makubaliano ya kushirikiana.

 

“Awali ya yote Mheshimiwa. Rais Nyusi na rafiki yangu nakushukuru sana kwa kuja Chato karibu sana, Rais wa Msumbiji anafahamu Kiswahili, anayajua maisha ya Watanzania kwa hiyo ni rafiki wa Watanzania. Rais Nyusi alinipigia simu akaniambia anataka kuja Chato, alisikia mimi niko Chato akasema anataka tuje tuzungumze masuala ya maendeleo ya nchi hizi mbili.

 

“Ninawashukuru sana Wizara ya Afya kwa kuamua jiwe la msingi la hospitali hii ya rufaa Kanda Chato kuwekwa na Rais wa Msumbiji, Mheshimiwa Filipe Nyusi.

 

“Historia ya Chato ni ndefu, Mwaka 1967 aliyekuwa Rais wa kwanza Mwalimu Nyerere alifika Chato wakati huo bado kikiwa ni kijiji akafungua kiwanda cha Pamba cha Chato kilichojengwa kwa thamani ya milioni 2 wakati huo. Mwalimu Nyerere alitambua maeneo haya ya Chato ni ya wakulima wa pamba na ndiyo maana akaja kukifungua kiwanda mwaka 1967, tarehe 9 mwezi wa kwanza.

 

“Mwalimu Nyerere alianzisha mchango wa wananchi waliokuwepo pale katika dhana ya kujitegemea na yeye akachangia paundi 1000 ambayo ilikuwa sawa na shilingi 2000 za Tanzania kwa ajili ya kujenga Bandari ya Nyamirembe.

 

“Mimi nimezaliwa hapa, hapa ni nyumbani siku ya Baba wa Taifa alipokuja mimi nilikuwa darasa la kwanza kutoka shule ya msingi ya Chato, kwanza hata nilikuwa simuelewi elewi vizuri Mwalimu Nyerere.

 

“Mheshimiwa Rais (Filipe Nyusi) kwetu sisi Watanzania tunaiona hii ni zawadi kubwa ya wewe kukubali kuja kuweka jiwe la msingi la hospitali hii itakayohudumia Watanzania lakini kwa sababu itakuwa hospitali kubwa itakayohudumia na wananchi wa Msumbiji,” amesema Magufuli.

 

Aidha, Waziri wa Afya, Dkt. Gwajima amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda- yaChato ilikadiriwa kutumia sh. bil. 16, Serikali imeshatoa sh. bil. 14 ambapo ujenzi umekamilika kwa asilimia 90 na makabidhiano yanategemewa kufanyika mwezi Machi, 2021.

 

 

“Awamu ya pili ya ujenzi huu imeshaanza kwa jumla ya gharama ya shilingi bilioni 14 ambapo mpaka sasa Serikali imetoa shilingi bilioni 4.1 na utekelezaji wake umefikia asilimia 37.

 

“Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi zaidi ya milioni 14 ambapo kwa siku itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa kati ya 700 – 1000. Tunamshukuru Rais Magufuli kwa maboresho ya afya nchini ambayo yamesaidia kuharakisha matibabu bobezi na kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje kutoka wagonjwa 682 mwaka 2014/15 hadi wagonjwa 42 mwaka 2020,” amesema  Gwajima.

 

 

Leave a Comment