×

Rasmi: Chikwende Mali ya Simba

RASMI, Winga Perfect Chikwende raia wa Zimbabwe aliyekuwa anakipiga ndani ya Klabu ya FC Platinum ni mali ya Klabu ya Simba iliyo chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Seleman Matola.

Simba imemuona nyota huyo raia wa Zimbabwe kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Uwanja wa Taifa wa Zimbabwe.

Katika mchezo huo wa mtoano, Chikwende alimpa tabu Aishi Manula kwa kumtungua bao moja baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Simba chini ya kiongozi wao Joash Onyango na Pascal Wawa.

Pia alikuwepo kwenye mchezo wa marudiano uliochezwa Uwanja wa Mkapa na Simba ikashinda mabao 4-0 zama za Sven Vandenbroeck ambaye kwa sasa yupo zake Morocco baada ya kubwaga manyanga ndani ya Simba, Januari 7.

 

Chikwende anakuwa mchezaji wa pili kutambulishwa rasmi na Simba baada ya kumalizana na kiungo mkabaji Thadeo Lwanga ambaye tayari ameanza kuingia kwenye mfumo wa Simba.

Nyota huyo amesaini dili la miaka miwili ambapo kupitia Ukurasa wa Instagram wa Simba wameweka wazi kwamba lengo kupata saini ya nyota huyo ni kwa ajili ya malengo ya Klabu Bingwa Afrika.

 

Dakika 180 za Chikwende ndani ya Simba akiwatungua bao moja zimetosha kuwashawishi mabosi hao kuweka mkwanja wa mezani na kupata saini ya winga huyo.

Awali ilielezwa kuwa mabosi wa Azam FC walikuwa wanahitaji saini yake ila dau ambalo walitajwa inaelezwa kuwa lilikuwa la kishkaji jambo lililowafanya FC Platinum kuiweka kando ofa hiyo na kuwapa winga huyo Simba.

Leave a Comment