The House of Favourite Newspapers

Wagonjwa Wapya wa Saratani Waongezeka Tanzania

0

 

TANZANIA  kuna ongezeko la wagonjwa wapya wa Saratani wapatao 50,000 na inakadiriwa kuwa, ifikapo mwaka 2030 kutakuwa na ongezeko la asilimia 50 ya wagonjwa wapya wa saratani.

 

 

Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima, wakati wa uzinduzi wa idara ya magonjwa ya saratani, huduma za patholojia na mkataba wa mteja kwenye hospitali ya Benjamin Mkapa, iliyoko Dodoma.

 

 

Amesema kuwa ongezeko hilo kwa mujibu wa Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Tafiti za Saratani (IARC) na kuongeza kuwa takwimu za hapa nchini za 2018 zinaonyesha kuwa idadi ya wagonjwa wapya wa saratani ni 14,028 sawa na asilimia 33.3 ya wagonjwa wote nchini.

 

 

“Saratani kama moja ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza inashika nafasi ya tano kwa wanaume na ya pili kwa wanawake kwa kusababisha vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza nchini,” alisema.

 

 

Kwa ujumla saratani zinazoongoza kwa wanawake ni mlango wa kizazi na saratani ya matiti. Kwa wanaume, saratani zinazoongoza ni Saratani za Tezi Dume, Koo pamoja na Kichwa na Shingo.

 

Aidha,  amesema Magonjwa ya Saratani yanatibika iwapo tu mgonjwa atawahi kupata tiba katika Vituo vya Afya vinavyotoa huduma hiyo. Zaidi ya asilimia 75 ya wagonjwa wa Saratani hufika katika Vituo vya Matibabu wakiwa wamechelewa sana na kuwawia vigumu madaktari kutibu na kuponya ugonjwa huo.

 

 

“Nitoe rai kwa wananchi, tujenge tabia ya kupima afya zetu mara kwa mara ili ikibainika kuwa tuna changamoto za kiafya basi tuanze matibabu bila kuchelewa,” alisisitiza Dkt. Gwajima.

 

 

Aidha, amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau na mashirika yasiyo ya Kiserikali imeendelea kuhakikisha inapambana na magonjwa ya saratani, ambapo katika kukabiliana na hilo Serikali imefunga mashine mbili za kisasa za tiba ya saratani kwa njia ya mionzi aina ya LINAC katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ambazo zimeanza kutoa huduma tangu Septemba, 2018.

 

 

Dkt. Gwajima aliongeza kuwa Serikali imeanzisha vituo takribani 624 ambavyo huweza kugundua na kutibu mapema saratani ya mlango wa kizazi.

Na WAMJW-Dodoma

Leave A Reply