Dhana ya kujenga mwili imezoeleka miongoni mwa vijana na wanamichezo hasa wanaume, lakini ukiingia kwa undani suala la kujenga mwili ni la wote wanaume na wanawake bila ya kujali umri ilimradi tu mwili wako una afya ya kutosha ya kuhimili mazoezi.
Mwili unajengwa tangu utotoni kwa kufuata mahitaji yake muhimu ambayo ni chakula bora. Kujenga mwili kunahitaji zaidi vyakula vya protini na vyenye kutia nguvu mwilini, vyakula hivi tutakuja kuviona katika mfululizo wa makala zetu.
Kujenga mwili Body building hutokana na mfululizo wa mazoezi ya nguvu za kuupambanisha mwili kwa lengo la kudhibiti na kuendeleza misuli ya mwili, mtu anayefanya mazoezi haya huitwa mjenga misuli au mjenga mwili.
Mazoezi haya husaidia mwili kuwa na nguvu na stamina na kuepuka kuanguka, kuumia au kuchoka kila wakati pia hufanya akili iwe timamu na nidhamu kwa ujumla.
Mtu huweza kufanya mazoezi haya kwa faida yake mwenyewe kwa ajili ya afya, au mwingine anataka kushiriki mashindano ya kitaifa na kimataifa au kuwa tu mtunisha misuli.
Unapofanya mazoezi haya, maji mengi hupungua mwilini, mafuta aina zote hasa nishati za mwili hupungua, hivyo huufanya mwili kuhitaji zaidi maji na nishati huku protini ikihitajika kuujenga mwili.
AINA ZA UJENGAJI WA MWILI
Watu wanaofanya mazoezi ya kujenga mwili hufanya hivyo kwa malengo ya kuwa na nguvu na mwili wenye mvuto, kuonekana watanashati na vijana.
Ujengaji wa mwili umegawanyika katika makundi matatu, kwanza ni wale waliobobea na wamefanya hiyo ndiyo kazi yao na huitumia kama sehemu ya ajira kwa kushiriki mashindano, kuwa mabaunsa na walimu kwa wengine wanaotaka kujenga miili.
Kundi la pili ni ambao miili yao inajengeka au wanaijenga kwa mazoezi ya kawaida, bila kutumia virutubisho vyovyote na pia kutumia fursa hiyo ya miili yenye nguvu kushiriki michezo na mashindano na kazi hii siyo sehemu ya kipato bali tu kuonekana nadhifu.
Kundi la tatu ni wanawake, hili ni maalum na la pekee, kwani kwenye jamii huonekana mwanamke mwenye nguvu na mtunisha misuli ni kivutio pekee, wanawake wa aina hii wapo wachache na wapo walioshinda mashindano ya kimataifa na wanajulikana sana.
Mazoezi ya kujenga mwili pia huwasaidia hasa Models wale wanaoshiriki mashindano ya mitindo kuwa na maumbo mazuri kwa wanawake na wanaume kwani kuna aina mbalimbali ya mazoezi haya kulingana na mahitaji ya mtu aonekane vipi.
JINSI YA KUJENGA MISULI
Ili kuweza kujenga mwili wako vizuri kimisuli kuna hatua tatu lazima uzipitie, lakini kama utahitaji kushiriki mashindano basi kuna hatua ya nne.
Hatua hizi ni kama zifuatazo; kwanza ni Cutting and bulking endapo utafuata vizuri hatua hizo mwili wako utaonekana umejengeka kimisuli vizuri na kwa muda mrefu, usipofuata ndipo hapo utaona kila ukifanya mazoezi mwili haujengeki ila unatokeza kitambi.
Kwanza hakikisha unaondoa mafuta yote mwilini hali iitwayo kitaalam Cutting kwa kufanya mazoezi ya kukimbia na kupunguza kwa kiasi kikubwa vyakula vyenye asili ya mafuta kama nyama. Katika hili pia kuna Bulking phase, hapa unatakiwa uhifadhi nishati ya kutosha mwilini ili usichoke haraka wakati wa mazoezi ya kupunguza mafuta.
Hapa tumia Glucose au vinywaji vyenye Glucose siyo Caffeine na kula chakula cha wanga kwa kiasi. Ukila chakula cha wanga kwa wingi kama wali na ugali utarudishia mafuta mwilini hivyo utashindwa lengo lako.
Ni vizuri kupunguza mafuta kwa kiasi kikubwa ili kutoa nafasi kwa misuli kutanuka. Hakikisha unapata protini ya kutosha ili kujenga misuli vinginevyo utajikuta unakonda kadiri unavyoendelea na mazoezi na kujinyima wanga.
Itaendelea wiki ijayo.