×

Shigongo Aendelea Kumwaga Vifaa Kwa Wanafunzi – (Pichaz + Video)

 

MBUNGE wa Buchosa, Mhe. Eric Shigongo, kupitia kampeni yake ya BUCHOSA MPYA, PELEKA MTOTO SHULE ameendelea na zoezi la ugawaji wa sare za shule na madaftari kwa wanafunzi ambao wanatoka katika familia zisizo na uwezo.

 

 

 

Baada ya kugawa vifaa hivyo katika Shule ya Msingi Katwe, Shigongo kupitia kamati yake ya hamasa, amegawa tena vifaa hivyo kwa wanafunzi wa shule nyingine mbili ambazo ni Shule ya Msingi Iligamba  na Shule ya Msingi Bupandwamhela.

 

 

 

Mbali na kugawa vifaa hivyo kwa watoto wanaotoka katika familia zisizo na uwezo, Shigongo pia ameendelea kugawa madaftari kwa kila mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule zote za Jimbo la Buchosa. Mpaka sass, jumla ya wanafunzi 46 wanaotoka kwenye familia zisizo na uwezo wamepatiwa sare za shule  na madaftari, huku akigawa jumla ya madaftari 1,930 kwa wanafunzi wa shule mbalimbali kwenye kata hizo.

 

 

 

Katika kuhakikisha wazazi na wanafunzi wanahamasika kwenda shule, mwakilishi wa Kamati ya Hamasa ya Buchosa Mpya, Mpeleke Mtoto Shule, Charles Matiku amesema kipindi cha kampeni Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo alikuwa akipokelewa na idadi kubwa ya watoto huku wakimueleza maombi yao kuhusu kuwasaidia suala la elimu, jambo ambalo aliwaahidi kutoa msaada kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika jimbo hilo likiwemo kundi la watoto.

 

 

 

Matiku amesema lengo la Mbunge Shigongo ni kuona Jimbo la Buchosa linakuwa na maendeleo mazuri katika kila nyanja na  ili kufikia malengo hayo lazima watoto waende shule kusoma, hiyo ndiyo itakuwa njia pekee ya kuwasaidia watoto hao kutimiza ndoto zao na kulisaidia taifa hapo baadaye.

 

 

 

Zoezi hilo endelevu limeanza jana Alhamisi, Januari 21, 2021, katika shule mbalimbali za msingi jimboni humo kwa kamati hiyo kushirikiana na madiwani, walimu wa shule husika na serikali za vijiji ikiwa ni wiki chache tangu kufunguliwa kwa shule za msingi na sekondari kote nchini.

 

 

 

Aidha, ameongeza kuwa lengo kubwa la kampeni hiyo iliyopewa jina la Kampeni ya BUCHOSA MPYA, PELEKA MTOTO SHULE na kauli mbiu yake ya ELIMU BORA KWA KILA MTOTO, ni kutoa hamasa kwa wazazi kuwapeleka watoto wao shule ili wakapate elimu na watoto hao kusoma kwa bidii kwa manufaa yao ya baadaye na taifa kwa jumla pamoja na kuhamasisha kuinua kiwango cha elimu katika jimbo hilo.

 

 

Matiku ameongeza kuwa Mhe. Shigongo amedhamiria kuleta maendeleo ya kweli katika Jimbo la Buchosa ikiwa ni pamoja na kuinua kiwango cha elimu katika shule za msingi na sekondari jimboni humo, hivyo wazazi wanao wajibu mkubwa wa kuwapeleka watoto wao shule na kuwahimiza katika masomo yao ambapo serikali nayo itafanya wajibu wake wa kupeleka miundombinu ya elimu, kuajiri walimu na kuendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji na kujifunzia ili kuiinua Buchosa kielimu.

 

 

Zoezi hilo litaendelea katika kata zote 21 na vijiji vyote 84 vya Jimbo la Buchosa mpaka pale watoto wote wenye uhitaji watakapopata mahitaji yote muhimu yatakayowawezesha kuanza/kuendelea na masomo yao.

 

 

 

 

 

 

 

 

SHIGONGO AANZA ZOEZI LA KUGAWA SARE ZA SHULE KWA WANAFUNZI

Leave a Comment