×

Kiungo Stars: Tutafia Uwanjani Dhidi ya Guinea

KIUNGO mkabaji wa timu ya taifa, Taifa Stars, Baraka Majogoro, amefunguka kuwa wamejipanga kupambana kwa nguvu kubwa kuhakikisha wanawafunga Guinea na kutinga hatua ya robo ya kombe la Chan.

 

Majogoro ameongeza kuwa akili yao kwa sasa wameielekeza katika mchezo huo wa mwisho wa Kundi D.

Stars iliyoshinda bao 1-0 dhidi ya Namibia juzi, wanashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Kundi D wakiwa na pointi tatu wakizidiwa pointi moja na Zambia na Guinea ambao ni vinara.

 

Stars wanaofundishwa na kocha Etienne Ndayiragije, wamebakisha mechi ya mwisho dhidi ya Guinea ambayo itaamua timu mbili ambazo zitaenda hatua ya robo fainali. Mechi hiyo itachezwa Jumanne ijayo.

Majogoro ambaye anaichezea Mtibwa Sugar ameliambia Championi Jumatatu, kuwa wana imani wakijitoa na kupambana wana uhakika wa kusonga katika hatua ya robo fainali.

 

“Kwenye hiyo mechi ni lazima tufe nao hata kama watatutoa lakini siyo kirahisi.

“Lakini siamini kama wataweza kututoa, kivyovyote vile tutapita kwenda robo fainali kwani tutapambana vya kutosha uwanjani,” alimaliza Majogoro.

Said Ally | Championi

Leave a Comment