×

JPM Ampa Maagizo Mazito Mwigulu – Video

 

RAIS  John Magufuli ameitaka Wizara ya Katiba na Sheria kuhakikisha Kiswahili kinatumika katika kesi na hukumu za mashauri mbalimbali hapa nchini kama lugha-mama kwani wananchi wengi wanakielewa na ndiyo lugha ya taifa badala ya kutumia Kingereza ambayo imekuwa kikwazo kwa baadhi ya wananchi.

 

Magufuli amesema hayo leo Jumanne, Februari 2, 2021, wakati akihutubia baada ya kumaliza kumwapisha aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Jaji Zepharine Nyalugenda Galeba, ambaye alimpandisha cheo jana na kumteua kuwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani baada kuandika hukumu kwa Kiswahili.

 

“Labda nikuulize Mwigulu, imagine baba yako ana miaka 88, Mzee Nchemba yuko Singida akawa na kesi na hukumu yake itolewe Kiingereza, imagine (fikiria) baba yako wa Kinyiramba atakavyohangaika, najua hajui Kiingereza atafanyaje na wizara unayoiongoza wameshatandika maneno ya Kingereza? Sanasana atakuja kwako apate tafsiri.  Kalisimamie hili.

 

 

“Ni lazima hili tujiulize kwamba kwenye Wizara ya Sheria na Katiba kuna tatizo… Wizara hii nimetoa kibali cha kuajiri wafanyakazi wa mahakama 200 mpaka leo hawajaajiriwa, waziri upo, katibu mkuu upo, AG (mwanasheria mkuu) upo.

 

 

“Wananchi wanalia kwa hukumu za Kiingereza ambazo hawawezi kuzisoma, kutafsiri tu lazima alipe pesa, tunatengeneza mateso na machozi kwa wananchi wengi muwaonee huruma Watanzania.

 

 

“Nitafurahi siku moja hata niende Mahakamani kusikiliza kesi ya mtu mwingine ambayo hainihusu mimi na hukumu yake itoke kwa Kiswahili, mtakuwa mmefanya mapinduzi makubwa. Jaji Mkuu Watanzania watakuheshimu kwa historia, umefanya mengi lakini hili limalizie.

 

 

“Mahakama ndio final (mwisho), unapoona mahali ambapo ni final halafu mtu anaondoka na lugha (hukumu) ambayo haijui (Kiingereza) kwa maoni yangu naona Mahakama inashiriki kumnyima haki mhusika.  Wote tumezaliwa vijijini ukiondoa wachache, kule wengine hawajaenda shule, tubadilike.

 

 

“Mahakamani mshtaki na mshtakiwa wanaongea Kiswahili, mashahidi wanaongea Kiswahili, wazee wa mabaraza, jaji/hakimu wanaongea Kiswahili lakini ikifika wakati wa kuandika mwenendo wa kesi au hukumu inaandikwa kwa Kiingereza.  Hii inawanyima haki na kuwaongezea gharama wananchi,” alisisitiza Magufuli.

 

 

Leave a Comment