
KLABU ya Simba leo Februari 5, 2021, imeingia makubaliano na Wizara ya Maliasili na Utalii ya kutumia neno VISIT TANZANIA kwenye jezi ambazo zitatumika katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo makubaliano hayo yamefanyika, makao makuu ya nchi, Dodoma.
Simba wanalazimika kutoa logo ya mdhamini wao mkuu “SportPesa” sababu Shirikisho la Soka Afrika CAF hawaruhusu timu shiriki kuwa na mdhamini shindani. Kampuni ya kubashiri ya 1Xbet ni wanadhamini michuano hiyo ya ligi ya mabingwa Afrika.

Akizungumza mara baada ya makubaliano hayo, Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez, amesema wao kama Simba wamefikia uamuzi huo kwa kutambua kwamba wana wajibu wa kuwa mabalozi wa kuitangaza nchi kupitia nafasi ambayo wameipata kwenye michuano hiyo mikubwa ya ngazi ya vilabu barani Afrika.
“Kwa kutumia maneno ‘Visit Tanzania’ ikiwa na maana ya Tembelea Tanzania kwenye jezi zetu, tunaamini kwamba itavutia watu wengi kutembelea nchi yetu kutoka kwenye mataifa mbalimbali,” amesema Gonzalez.