
JACKSON BAHATI (27), mkazi wa kijiji cha Buhangizi, Kata ya Kagu, mkoani Geita, anadaiwa kuwajeruhi watoto wake wawili kwa kuwachoma kisu maeneo ya tumboni baada ya kwenda kijiji jirani na kumkuta mke wake ameolewa na mwanamme mwingine.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi (ACP) Dismas Kisusi, akithibitisha jana tukio hilo amesema kuwa tukio lilitokea majira ya saa 9:00 usiku Januari 27, mwaka huu.
Alisema baada ya kutenda kitendo hicho, mtuhumiwa naye alijichoma kisu mara nne kwenye tumbo lake na kisha kunywa sumu ya panya kwa lengo la kujiua.
Kamanda Kisusi aliwataja watoto waliojeruhiwa kuwa ni Leah Jackson (4) na Bahati Jackson (3) ambao wote walichomwa kisu maeneo ya tumboni na baada ya kutokea kwa tukio hilo, walipata msaada kutoka kwa raia wema na kupelekwa Hospitali ya Nzera na hadi sasa hali zao zinaendelea vizuri.