
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Mkuu wa Wilaya kuhakikisha uozo unaoendelea kwenye Soko Kuu Jipya la Morogoro ukome mara moja.
Magufuli ametoa agizo hilo kwenye hotuba yake leo Februari 11, 2021 wakati akizindua soko hilo la kisasa mkoani Mororgoro.

”Nimepata ushahidi kuwa kodi ya vizimba ni elfu 20 kwa mwezi, lakini kuna wafanyakazi wa Manispaa wanawatoza elfu 50, hizo pesa wazitapike mara moja na wananchi waanze kulipa gharama ya elfu 20 tu, nasisitiza hizo elfu 30 walizokula wazitapike.

”Nasikia Mkuu wa Wilaya eti hili nalo anaunda kamati tena ilipwe, wakati unaweza kusimama tu pale nje ukagundua watu wanatozwa pesa zaidi, sasa nakuagiza Waziri wa TAMISEMI huu uozo unaoendela hapa ukome mara moja.”” – Magufuli
“Leo nimeamua kuja hapa (Morogoro) wasaidizi wangu walikuwa wamenipangia nipitilize nimesema nalala hapa leo ili nijue yaliyomo humu ndani na kero za wananchi wangu.

“Nimeamua kulala hapa Morogoro, nawaomba radhi sana wasaidizi wangu, lakini lazima nilale hapa niweze kusikiliza kero nyingine ili tuzimalize na hata kama kuna miradi yoyote mingine mimi kesho nipo tayari kuizindua.

“RC wa Morogoro na DC haiwezakani mambo ya hovyo yanafanywa na ninyi mpo hapa, ninyi ndio mnaniwakilisha mimi, TAKUKURU kweli hamuoni hii rushwa? Kama mfanyakazi wa Manispaa anakula Elfu 30 (cha juu) kila mwezi kwa kutumia jengo la Serikali hiyo sio rushwa?

“Uongozi wa Morogoro ukoje? Najiuliza maswali mengi, nasikia DC anaunda Tume, Tume yanini? Ukahangaike kuunda Tume ya kuchunguza hili (rushwa kwenye soko), si ingia hapo ndani uchukue kibanda ukae uangalie kwa masaa tano utaona tu, mpaka Tume ukailipe hela na posho?

“Nataka uozo uliomo humu kwenye Soko Kuu la Manispaa ya Morogoro kuanzia leo ukome, Waziri wa TAMISEMI, RC, DC, DED, Mbunge na wengine mkalishughulikie hili na nisilisikie tena, kama ni Elfu 20 hiyohiyo, nataka Wafanyabiashara wadogo wawe Mabilionea.

“Na wewe Mstahiki Meya wa Morogoro ubadilike, najua umeupata Umeya kwa bahati bahati sana, hukutakiwa kuwa Meya, aliyetakiwa sikumrudisha kuwa Meya, hata utafutaji wa Meya hapa ulijaa rushwa ndio maana Katibu wa CCM wa hapa tumemsimamisha kazi, alikula rushwa kwa Madiwani.

“Udiwani ni Utumishi, hamuwezi kuwa mnapitisha Sheria ndogo za kuwaumiza waliowapigia kura, tuzingatie Sheria bila kuwanyanyasa Watu, DED Morogoro hakuna cha By Law, hakuna cha By nini, fuata Sheria Watoza ushuru wako hapa Sokoni wafukuze wakatoze ushuru kwenye vyoo Mjini.

“Nawaambia Watu wa Bodaboda hawaruhusiwi kuingia hapa kwenye Soko la Manispaa ya Morogoro, sasa mnunuzi wa nyanya atakuja kwa miguu azibebe begani nyanya zake? Kama parking ya Magari, Bajaji na Pikipiki kwanini mnawazuia ku-park?” amesema Magufuli.