
KOCHA Mkuu wa Simba, Mfaransa, Didier Gomes, amepanga kukifumua kikosi chake kitakachoivaa AS Vita ya DR Congo katika mchezo wao wa kesho wa hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mchezo huo wa Kundi A unatarajiwa kupigwa saa saa 1:00 usiku pale Stade des Martyrs, Jiji la Kinshasa, DR Congo. Simba imepangwa kundi hilo na timu za Al-Merrikh, Al Ahly na AS Vita.
Akizungumza na Spoti Xtra, Gomes alisema kuwa upo uwezekano mkubwa wa kuwepo mabadiliko katika safu yake ya kiungo ambayo awali alikuwa akiwatumia Taddeo Lwanga, Mzamiru Yassin na Said Ndemla.

Gomes alisema katika mchezo wa kesho, safu ya kiungo anaweza kumtumia mkongwe Erasto Nyoni na Lwanga katika kuhakikisha wanapunguza mashambulizi golini kwao.
Mfaransa huyo alisema kuwa AS Vita watataka kutumia vema uwanja wao wa nyumbani kwa kushambulia, hivyo ili kuwapunguza kasi amepanga kuwatumia viungo wengi wakabaji.Aliongeza kuwa safu yake ya ulinzi itakuwa na mabadiliko kwa kumuingiza kikosini Joash Onyango raia wa Kenya ambaye hakuwepo katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam.
“Tarajieni kuona mabadiliko makubwa katika kikosi changu kuelekea mchezo dhidi ya AS Vita, tunafahamu umuhimu mkubwa wa mchezo huu wa kigeni, kikubwa nimetaka wachezaji wangu kutumia vema katika kila nafasi tutakayoipata.

“Kikubwa hatutaki kufanya makosa tuliyoyafanya katika mchezo wa mwisho wa ligi tuliocheza dhidi ya Azam ambao wachezaji wangu walishindwa kutumia vema nafasi zaidi ya nne za kufunga mabao.
“Katika kuelekea mchezo huo wapo baadhi ya wachezaji hawapo kwenye mipango yangu kati ya hao ni Mkude (Jonas) ambaye yeye bado hajawa fiti kwa ajili ya mapambano, kama kumtumia labda mchezo wa marudiano.“Kabla ya safari ya kuelekea DR Congo, juzi tulicheza mchezo wa kirafiki na kikosi cha vijana cha U20, nilimtumia Mkude kwa ajili ya kumuangalia nikamuona hana mechi fitinesi lakini ni mzuri.“
Pia nilimjaribu Nyoni kucheza nafasi hiyo ya kiungo nilimuona yupo vizuri na kuongeza kitu kwenye eneo hilo, hivyo huenda akaanza kucheza pacha na Lwanga,” alisema Gomes.
MBINU ZA KUIUA AS VITA
Katika mchezo huo wa kesho, Simba imepanga kutumia mbinu za kushambulia na kujilinda kwa umakini ili tu kufanya vizuri mbele ya wapinzani wao hao.
Hilo limewekwa wazi na Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola akisema:
“Kila mchezaji yupo tayari na tunajua kazi ni ngumu kimataifa ila hatuna mashaka kutokana na kuwa na muda wa maandalizi pamoja na ushirikiano ambao upo ndani ya timu.“Ushindi ni mbinu, ili ushinde ni lazima ushambulie, hivyo tutashambulia kwa hesabu pia ni lazima tulinde lango letu liwe salama kwa kuwa ugenini inabaki kuwa ugenini tu.”

WACHEZAJI WALA KIAPO
Kwa upande wa wachezaji wa Simba, kuelekea mchezo huo wamekula kiapo kwa kuahidi kupamabana kufa na kupona kuhakikisha wanafanya vizuri dhidi ya AS Vita.
Kipa namba moja wa kikosi hicho, Aishi Manula, alisema: “Wachezaji wengi wa Simba wanakumbuka kila kitu kuhusu mchezo huu, tulipoteza kwa idadi kubwa ya mabao tulipocheza dhidi yao kipindi kile, lakini kila kitu kimebadilika kwa sasa na malengo yetu kama timu ni kufanya vizuri huku ushindi likiwa ndio lengo letu kubwa zaidi.
Nahodha msaidizi wa kikosi hicho ambaye ni beki wa kushoto, Mohamed Hussein, alisema: “Kikubwa kwetu ni kupata maombi ya wapenzi wote wa Simba kwani naamini tukishinda watapata furaha kubwa.

“Huu ni mchezo wa ugenini, kwa upande wetu tunahitaji matokeo ambayo yatakuwa mazuri kwetu, hatuna malengo ya kupoteza, tutapambana kwa nguvu zetu zote ili kupata ushindi.”
MIKAKATI YA VIONGOZI
Wakati jana mchana Simba ikiwa imefika DR Congo ikiwa imetoka Dar juzi Jumanne kupitia Addis Ababa, Ethiopia, uongozi wa Simba umesema umetua nchini humo kwa tahadhari kubwa kuhakikisha wanakwepa hujuma zote za wapinzani wao ikiwa ni pamoja na kujihadhari na matukio yaliyowahi kuwatokea huko nyuma pindi walipokwenda kucheza nchini humo.

Mwenyekiti mpya wa Simba, Murtaza Mangungu, amesema: “Kikosi kitaanza mazoezi muda mchache baada ya kupata mapumziko mafupi tayari kwa kujiandaa na mchezo huo, mipango yote iliyopangwa inakwenda sawa.“Kuhusu suala la hujuma, uongozi tumejipanga vyema na tulitanguliza watu wiki moja kabla kwa ajili ya kuandaa mazingira mazuri kabla ya kikosi kwenda, hivyo kila kitu kinakwenda sawa pia tunakwenda na tahadhari kwani kuna vitu vingi tulifanyiwa huko nyuma tumevidhibiti, hivyo tunatarajia ushindi.”