
PENGINEwatu wengi watakuwa wamesahau kidogo kilichotokea Februari 12, 2019 pale Uwanja wa Mkapa jijini Dar, lakini Al Ahly, wana kumbukumbu zote na wamekuja hapa nchini kwa lengo kubwa la kusahihisha makosa yao.
Al Ahly ambao usiku wa kuamkia jana Jumamosi walitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar, keshokutwa Jumanne watakuwa wageni wa Simba kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar ukiwa ni mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Waarabu hao wanakumbuka mara ya mwisho kucheza hapo na Simba ilikuwa Februari 12, 2019 katika hatua kama hii na wakapoteza kwa bao 1-0 lililofungwa na Meddie Kagere dakika ya 65 kwa shuti kali akiwa ndani ya boksi baada ya kupokea pasi ya nahodha, John Bocco.

Mara tu baada ya kutua jijini Dar, kocha wa timu hiyo, Pitso Mosimane, alisema: “Sina cha kuzungumza zaidi, nitazungumza siku ya mkutano na wanahabari.“Nafahamu kwamba itakuwa mechi ngumu, mara ya mwisho Simba walitufunga (1-0), hivyo tumekuja kurekebisha makosa.
”WATUA NA WATU 70
Msafara mzima wa Al Ahly uliotua ulikuwa na watu 70 wakiwemo wachezaji 22. Katika wachezaji hao, yupo mshambuliaji Mzambia, Walter Bwalya ambaye aliwahi kutajwa kutakiwa na Simba.Spoti Xtra ambalo lililokuwepo uwanjani hapo, lilishuhudia timu hiyo ikitua saa 5 usiku, kabla ya kuanza kutoka ndani majira ya saa 6 baada ya kukamilisha taratibu za uingiaji nchini wakiwa na balozi wao wa hapa nchini ambaye ndiye aliongoza mapokezi hayo.
Msafara wa wachezaji na viongozi ulianza kutoka ukiwa umebeba shehena ya mizigo ambayo kwa mujibu wa watu waliowapokea walidai katika mizigo hiyo kuna vyakula na maji watakayotumia kipindi chote watachokuwa hapa nchini.Kutokana na ukubwa wa msafara wa timu hiyo, Spoti Xtra limeshuhudia gari tisa zilizofika uwanjani hapo kuwapokea likiwemo basi la wachezaji.
MWAMUZI HUYU HAPA
Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limemtaja mwamuzi wa mchezo huo kuwa ni Sidi Alioum raia wa Cameroon.Mwamuzi huyo mwenye uzoefu mkubwa wa kuchezesha mechi za kimataifa, ndiye aliyechezesha fainali ya AFCON 2019 ambayo Algeria iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Senegal, michuano iliyofanyika Misri.
IBRAHIM MUSSA, DAR