
RAIS John Magufuli ametoa wito kwa vyombo vya habari kuripoti habari na matukio kwa weledi badala ya kuripoti taarifa kwa ushabiki bila kuwa na uzalendo wa kweli kwa taifa lao.
Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, katika viwanja vya Mnazi Mmoja wakati akilihutubia taifa baada ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Soko Kuu la Kisutu jijini Dar es Salaam.
“Serikali katika miaka mitano imeimarisha ipasavyo haki na wajibu wa vyombo vya habari. na kuhakikisha vinatoa haki na kuthamini suala la kutoa haki katika mambo ya habari. Mwaka 2015 kulikuwa na vituo vya redio 106 tu katika nchi nzima, lakini hadi mwezi Februari 2021, tuna vituo vya redio sasa 193.

“Natoa wito kwa Wanahabari tutangulize uzalendo, kumekuwa na habari nyingi za uzushi, mara fulani kafa, vigogo wafa, vigogo wapukutika ni mambo ya ajabu, tumefikia Watanzania tunaombeana kufa, taarifa ambazo nchi yetu inachafuliwa unakuta watu wanashabikia.

Katika Mkutano wa Hadhara wa Rais Magufuli uliofanyika Mnazi Mmoja Dar es Salaam. Rais ametoa wito kwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa waaminifu katika kazi zao.
Amesema kuna watumishi huwa wanawakadiria wafanyabishara kodi kubwa sana na wanaposhindwa kulipa basi hutaka kugawana kile kiasi kidogo ambacho mfanyabiashara anakuwa nacho.
Amewataka TRA wajifunze kutoa haki kwa wafanyabishara ambao wanania ya kulipa kodi. Amesema TRA kuna wafanyakazi wala rushwa, hivyo ni lazima wajirekebishe. Ameiambia Wizara ya Fedha kuwa wakasimamie suala hilo, kwa kuwa nchi inahitaji kodi, inahitaji ushuru lakini uwe wa haki.