
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekabidhi vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 357 kwa vikundi vitano vya wajasiriamali vilivyotolewa kwa mkopo na Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa ikiwa ni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.
Pia, Waziri Mkuu amepokea msaada wa madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni 10 kutoka katika Kampuni ya vinywaji baridi ya Cocacola Kwanza ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini.

Waziri Mkuu amekabidhi vifaa hivyo (Jumamosi, Februari 27, 2021) katika viwanja vya shule ya msingi Likangara wilayani Ruangwa na kuwataka wanufaika wa mikopo hiyo wakaitumie kama ilivyokusudiwa na wahakikishe wanarejesha kwa wakati.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kuamua kutoa mikopo ya vifaa mbalimbali kwa wajasiriamali na pia ameitaka ihakikishe inawasimamia vizuri wanufaika hao