
KUNA msemo wa kimila usemao: “Tembo wakianguka huinuana.” Hiki ndicho kinachoonekana kwenye skendo inayomhusu msanii wa Bongo Fleva, Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ na mtoto msanii wa Bongo Muvi, Kajala Masanja, Paula Paul kuhusu ishu ya video yao chafu kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ambayo inadaiwa vigogo (majina kapuni) wameizima tayari.
Vyanzo vya habari na uchunguzi wa Timu ya Risasi umebaini kuwa kuna msululu wa vigogo wa kada mbalimbali ambao wamejitolea kuzima ishu hiyo kibabe kwa kuwaambia wahusika: “Achaneni na chokochoko.”
ISHU ILIANZIA HAPA
Februari 13, mwaka huu video chafu ya Rayvanny na Paula ilirushwa kwenye mitandao ya kijamii na ikiwaonesha wakifanya mambo ya ‘kikubwa’ hadharani jambo ambalo lilimkasirisha mama wa binti huyo ambaye ni Kajala na kuweka wazi msimamo wake wa kulifikisha jambo hilo kwenye vyombo vya sheria.
Mapema kabla tukio halijapoa Kajala alimtuhumu shoga yake Hamisa Mobetto kuwa ndiye aliyehusika kumkuwadia mwanaye kwa Rayvanny, jambo ambalo Mobetto alilikanusha kwa kumwandikia barua ya wakili Kajala akikusudia kumchukuliwa hatua za kisheria kwa kumchafulia hadhi yake kwenye jamii.
Februari 15, mwaka huu msanii Rayvanny ambaye ni nguli wa muziki kutoka lebo ya Wasafi Classic Baby ‘WCB’ inayomilikiwa na msanii nyota Bongo, Nasibu Abdul ‘Diamond’ alionekana kwenye kituo cha polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam na habari zikadai kuwa alikwenda kuhojiwa kuhusiana na skendo ya video yake chafu iliyoonesha akimfanyia mambo ya ‘utundu’ Paula.
UKIMYA WATANDA
Tangu msanii huyo adaiwe kuhojiwa na vyombo vya dola na polisi kukiri hadharani kuanza uchunguzi juu ya tukio hilo, mambo yamekuwa kimya na kwamba hakuna upande unaoonekana kusema chochote.
Kajala ambaye mwanzo alionekana kuwaka kinomanoma kuhusu mwanaye kuchezewa na Rayvanny alipoulizwa na waandishi wetu nini kinaendelea kwenye sakata la mwanaye alisema: “Mimi nimeviachia vyombo vya dola.”
Hata hivyo, uchunguzi wa waandishi wetu umebaini kuwa, kuna baadhi ya vigogo serikalini kwa kushirikiana na mabosi wa lebo ya WCB wamekuwa wakihaha kuimaliza skendo hiyo kimyakimya.
“Unadhani kuna ishu tena, imeshamalizika kuna …(majina yanatajwa, sisi tunayaficha kwa sababu maalum) wameomba mambo yaishe,” chanzo chetu kilidai.
HUYU HAPA KAMANDA WA POLISI
Wandishi wetu walipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai kumuuliza wamefikia wapi kuhusu sakata la Rayvanny na Paula alisema: “Bado uchunguzi unaendelea na wanasheria wanaangalia kama kuna jinai.”
Chanzo chetu kingine kilicho karibu na ‘Timu msaidiea Rayvanny’ kilidai kuwa, tayari mpango wa kuwakutanisha Kajala, Paula, Rayvanny na Mobetto upo tayari na wakati wowote mambo yatakwishi.
MOBETTO ANASEMAJE?
Rafiki wa karibu na Mobetto alimwambia mwandishi wetu kuwa mwanamitindo huyo naye ameshaachana na mpango wake wa kumfikisha Kajala mahakamani na kwamba yuko tayari kuyamaliza kishkaji.
“Si unakumbuka Hamisa alimpa Kajala saa 24 za kufuta posti yake aliyomtuhumu mtandaoni na kumuomba radhi; yote hayo hayajafanyika lakini unaona Hamisa amesema kitu? Hamisa anaendelea na maisha yake,” rafiki huyo alisema.
HII HAPA HATARI YA RAYVANNY KUTUPWA JELA
Kwa mujibu wa wanasheria mbalimbali ambao wamelitazama tukio hilo kupitia kipande cha video ya Paula na Rayvanny iliyovuja wanasema, huwenda msanii huyo akashtakiwa kwa makosa matatu. Kosa la kwanza ambalo wanasheria hao wanasema linaweza kumkabili Rayvanny ni la kufanya mapenzi na mwanafunzi ambapo inaelezwa kuwa Paula angali anasoma Kidato cha Tano.
Wanasema, endapo atakutwa na hatia hii msanii huyo atafungwa miaka kati ya mitano hadi saba au kulipa faini. Kosa la pili ambalo linaweza kumtia matatizoni msanii huyo ni la makosa ya mtandao kwa vile video yao yenye maudhui ya kudhalilisha ilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Inaelezwa kuwa Rayvanny akikutwa na kosa hili anaweza kulipa faini ya shilingi milioni tano, au kifungo cha miaka mitatu jela au vyote kwa pamoja. Na kosa la mwisho ni la ubakaji hasa ikibainika kwamba kabla ya kufanyiwa ukatili huo binti huyo mwenye umri wa miaka 19 hakufanya hayo kwa ridhaa yake.
“Hayo ndiyo makosa ambayo kwangu mimi nikiangalia yanaweza kuwa na mashiko endepo ushahidi wa kutosha utapatika, kama ikibainika alibaka adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela” alisema mwanasheria Amran Msami alipozungumza na mwandishi wetu.
Pengine kwa kuzingatia mtego huo wa kisheria ndiyo maana vigogo wamehaha kumuokoa msanii huyo yasimfike mazito na kumharibia malengo yake ya kimaisha katika muziki.
Stori | Mwandishi Wetu, Risasi