
WAKATI Yanga ikisaka kocha mkuu mpya, taarifa zinasema kwamba, Kaimu Kocha Mkuu timu hiyo, Juma Mwambusi, amekuwa kwenye vikao vya kupendekeza ni kocha gani afanye naye kazi na kufunga mjadala uliopo wa nani ni mrithi wa Cedric Kaze.
Hivi karibuni, uongozi wa Yanga, ulitangaza kuvunja benchi la ufundi la timu hiyo lililokuwa likiongozwa na Kocha Mkuu, Cedric Kaze raia wa Burundi kwa kile kilichoelezwa ni kutoridhishwa na matokeo.
Sasa katika kikao cha kujadili kocha gani atue ndani ya kikosi hicho, Mwambusi na viongozi wengi wa juu wa klabu hiyo, wamependekeza jina la kocha wa zamani wa Township Rollers ya Botswana, Nikola Kavazovic raia wa Serbia.

Licha ya wengi kumchagua kocha huyo, lakini pia baa-dhi ya viongozi wa timu hiyo wamekuwa kwenye mazungumzo na Kocha Mfaransa, Hubert Velud.
Hurbert amewahi kuzinoa TP Mazembe ya DR Congo, Etoile du Sahel ya Tunisia, ES Setif na USM Alger zote kuto-ka Algeria, hivyo ana uzoefu mkubwa na soka la Afrika kama ilivyo kwa Kavazovic aliyepitia Township Rollers, AFC Leopards na Free State Stars.
Spoti Xtra limedokezwa kuwa, Mwambusi amemchagua Kavazovic, wakati huu yeye akiendelea kukinoa kikosi hicho kwa muda akimsubiri mkubwa wake aungane naye.

“Hakika viongozi wetu wanaonekana kutumia busara kubwa sana katika mabadiliko haya ya kiufundi yaliyotokea baada ya hivi karibuni kulivunja benchi lote la ufundi, kwani huwezi kuamini kocha wetu Mwambusi ni miongoni mwa watu waliohudhuria kikao cha kuchambua CV za kocha mpya na vilevile amepewa nafasi ya kuchagua benchi jipya la ufundi.“
Kama hali hii itaendelea nina imana kwamba timu haitayumba sana kwenye michezo ijayo, maana utulivu aliouonesha Mwambusi unawafanya hata wachezaji kuwa karibu naye.
“Hata kama kocha mpya akija, ninaimani kubwa hatakuwa na kazi ngumu maana tayari Mwambusi ame-ingia kambini,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo kingine kiliongeza kwamba: “Uongozi upo katika mazungumzo na moja kati ya makocha wakubwa barani Afrika anayefahamika kwa jina la Hurbert Velud, ni kocha ambaye amefundisha klabu kubwa Afrika kama TP Mazembe na Timu ya Taifa ya Togo.
“Ni kocha ambaye kama mambo yatakuwa mazuri basi ataifikisha Yanga sehemu nzuri kwa kuwa kote ambapo alipita aliacha alama ya mafaniko na soka safi la kuvutia.”
Spoti Xtra lilizungumza na Mwambusi ili kufahamu namna alivyoanza majukumu yake ndani ya kikosi hicho kwa mara nyingine ambapo alisema: “Tayari nipo kambini na wachezaji ambao hawajaitwa timu za taifa, kikubwa leo (juzi Ijumaa) nimeanza mazoezi na kwamba tutafanikiwa kurejesha utulivu kwa wachezaji wote.
“Kuna baadhi nimeanza nao kazi kama vile daktari, kocha wa viungo (Edem Mortotis), mchua misuli (Fareed Cassim) na meneja wa timu (Hafidh Saleh).”
NA MUSA MATEJA NA MARCO MZUMBE,Dar es Salaam