×

Prof. Lipumba: Tumebaki Wakiwa

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema Rais John Magufuli atakumbukwa kwa mengi ikiwemo ujenzi wa miundombinu na jinsi alivyowabana mafisadi.

 

 

Profesa Lipumba ambaye alikuwa miongoni mwa wagombea urais waliochuana na Magufuli katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka 2020 ameeleza hayo leo Alhamisi Machi 18, 2021 katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuhusu kifo cha kiongozi huyo kilichotokea jana Jumatano Machi 17, 2021.

 

 

“Kifo chake cha ghafla kinatia uchungu na simanzi kubwa. Amri ya Mungu haina makosa. Kila wakati kauli za Rais Magufuli zilimtanguliza Mungu. Mimi binafsi na CUF tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo chake kutokana na maradhi ya moyo, hakika Taifa limegubikwa na huzuni kubwa na giza nene.”

 

 

“Masikio yamepokea taarifa ambayo akili haiko tayari kuibeba wala kuikubali kwa kuzingatia uhalisia kwamba ni wiki tatu tu zilizopita Rais Magufuli alifanya kazi kubwa bila kuchoka kuzindua miradi mikubwa ya maendeleo ikiwa ni pamoja na daraja la Ubungo (Kijazi Interchange) na stendi mpya ya mabasi iliyopo Mbezi, Dar es Salaam. Tunamuomba ampe pumziko la amani,” amesema Lipumba.

 

 

Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, mara ya mwisho kuonana na ana kwa ana Rais Magufuli ilikuwa katika maadhimisho ya siku ya mahakama Februari Mosi, 2021 mjini Dodoma.

 

 

“Alinikaribisha bila mimi kutarajia nizungumze maneno machache kwenye hafla ile. Nilimkumbusha ahadi zake alizozitoa mwaka 2015 wakati akizindua Bunge la 11 ikiwa ni pamoja na kukamilisha upatikanaji wa Katiba Mpya.”

 

 

“Pia nikaeleza kuwa katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la 12 aliwagawia wabunge hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la 11 mwaka 2015 na akasisitiza kwamba yote ambayo hayakutekelezwa katika kipindi chake cha kwanza yatatekelezwa kwenye awamu ya pili,” amesema Lipumba.

 

 

Mwenyekiti huyo wa CUF amesema siku hiyo Rais Magufuli alionekana mwenye afya njema na mchangamfu,“ alinitania kwa kusema kuwa baada ya uchaguzi Profesa Lipumba amenenepa na aliupokea ujumbe wangu vizuri. Niliamini kabisa kiporo cha upatikanaji wa katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi atakifanyia kazi kwa dhati katika kipindi chake cha pili.”

 

 

Amesema CUF inatoa salamu za pole kwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, familia ya Rais Magufuli na Watanzania wote.

“Kwa hakika tumebaki wakiwa na ni vigumu kulizoea pigo hili la kwanza la aina yake. Pamoja na kuwapoteza marais wastaafu, hii ni mara ya kwanza kumpoteza rais akiwa madarakani,” amesisitiza.

 

 

Katika taarifa hiyo msomi huyo wa uchumi amesema kwa kuzingatia katiba ya nchi hususan Ibara ya 37 (5), Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ndiye atakayeapishwa kuwa Rais wa sita wa Tanzania.

“Tunamuombea kwa Mungu, utekelezaji mwema na wa haki wa majukumu yake utakaoliletea maendeleo na heshima Taifa letu,” amesema.

 

 

Amemtaka Samia kuenzi haki, umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kiwango cha juu kuliko nyakati zote pamoja kukamilisha ahadi za Rais Magufuli likiwemo suala la mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi.

Leave a Comment