
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Jumatano Machi 24, 2021 anawaongoza wakazi wa Mwanza na mikoa jirani kumuaga aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli.
Utoaji wa heshima za mwisho unafanyika katika uwanja wa CCM Kirumba uliofurika watu huku wengine wakifuatilia shughuli hiyo kupitia luninga nje ya uwanja.
Waombolezaji walioanza kuingia uwanjani hapo tangu saa 10 alfajiri huku baadhi wakiujaza uwanja wa ndege kuulaki msafara wa mwili wa Hayati Magufuli uliotokea visiwa vya Zanzibar.
Pamoja na mawaziri na naibu mawaziri, hafla ya kutoa heshima za mwisho kwa Dk Magufuli anayetarajiwa kuzikwa nyumbani kwake Chato Machi 26, 2021 pia imehudhuriwa na wakuu wote wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiongozwa na mkuu wa majeshi Jenerali Venance Mabeyo.
Baada ya shughuli ya uwanjani, jeneza lenye mwili wa Hayati Magufuli litazungushwa kwenye mitaa mbalimbali jijini Mwanza kabla ya safari ya kuelekea Geita kupitia Kigongo-Busisi.