
Hatimaye Rais wa Uganda Yoweri Museveni na mkewe mama Janet Museveni wamepata chanjo yao ya Covid-19. Mwanahabari wa Rais Yoweri Museveni Don Wanyama, amefahamisha katika mtandao wake wa kijamii wa Twitter kwamba Rais Museveni amepata chanjo hiyo aina AstraZeneca leo jumamosi katika Ikulu ya Nakasero mjini Kampala.
Taarifa hizo pia zimeonekana kwenye akaunti ya Twitter ya Rais Museveni. Rais Museveni amehamasisha raia wa Uganda ambao wapo kwenye kundi la wanaoweza kupata chanjo, kufanya hivyo katika mpango huo ambao upo kwenye awamu yake ya pili.
Uganda ilizindua chanjo ya Covid-19 tarehe 10 mwezi huu wa Machi, katika Hospitali kuu ya taifa ya Mulago mjini Kampala, baada ya kupokea shehena ya dozi 864 toka kwa mpango wa Covax na dozi laki moja kutoka serikali ya India na kuhitimisha dozi 964,000.
Awamu ya kwanza ilijumuisha wahudumu wa afya, maafisa wa usalama, walimu na wanahabari. Awali, Rais Museveni katika hotuba yake kwa taifa, alisema kuwa bado anatafakari ni chanjo gani ambayo atachanjwa na hatimaye leo amefanya maamuzi na kupata chanjo hiyo.
Hata hivyo, kuliwahi kutokea taarifa mwezi uliopita kuwa rais na watu wake wa karibu walikuwa wanapokea chanjo nyingine kwa siri kabla ya taifa hilo kupokea chanjo rasmi, taarifa ambazo Waziri huyo Jane Aceng, alikanusha.